Watumishi watano watumbuliwa

06Mar 2017
Hamisi Nasiri
MTWARA
Nipashe
Watumishi watano watumbuliwa

WATUMISHI watano wamesimamishwa kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa makosa tofauti likiwamo utoro kazini na matumizi mabaya ya rasilimali za serikali.

Tukio hilo lilitokea wakati wa kikao cha siku mbili cha Baraza la Madiwani na kikao cha kazi katika halmashauri hiyo katika kipindi cha robo ya pili cha kupokea taarifa za kata katika utekelezaji wake ndani ya kipindi hicho.

Madiwani hao walichukua uamuzi huo baada ya kushuhudia kwa kipindi kadhaa na kujiridhisha kuwapo kwa makosa dhidi ya watumishi hao licha ya jitihada za kuwaonya bila mafanikio.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Omari Kipanga alisema watumishi hao bila kuwataja majina watatu ni wa sekta ya afya na wawili ni watendaji wa vijiji.

Alisema watumishi wa afya wanakabiliwa na makosa ya utoro kazini kwa siku kadhaa huku watendaji wa vijiji wakikabiliwa na makosa ya kufanya matumizi mabaya ya mali za serikali.

Aliyataja maeneo waliokuwa wakifanyia kazi watumishi hao kuwa ni Kata za Moma, Mpapura na Nalingu katika halmashauri hiyo.
“Jitihada za kuwaonya watumishi hao zimefanyika sana, lakini bado wakawa wanakwenda kinyume cha taratibu za kisheria.

Sasa kupitia baraza hili, tumeona ni vema wakae pembeni ili kupisha wengine ambao wanahitaji kazi. Mfano; mtu anaondoka eneo lake la kazi ndani ya siku kadhaa bila taarifa,” alisema Kipanga.

Diwani wa Kata ya Nalingu, Shaibu Salumu, aliipongeza kamati ya fedha na mipango kwa hatua hiyo kwani watendaji hao wamekuwa hawana uaminifu kwenye utendaji wao wa kazi.

“Hii itakuwa fundisho kwa watendaji au watumishi wengine ambao watathubutu kufanya vitendo kama hivi na hali hii inarudisha nyuma maendeleo ya halmashauri na mkoa wetu kwa jumla,” alisema Salumu.

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Evod Mmanda, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia vema suala zima la elimu ikiwamo la watoto wenye sifa ya kwenda shule kuripoti bila kukosa kinyume na hivyo hatua za kisheria zitafuata.

Pia aliwataka kuweka jitihada mbalimbali katika sekta hiyo ya elimu ili kuwezesha uwapo wa matokeo mazuri katika halmashauri hiyo na mkoa kwa jumla.

Habari Kubwa