Watumishi watatu h’shauri wafukuzwa utovu nidhamu

02Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Sikonge
Nipashe
Watumishi watatu h’shauri wafukuzwa utovu nidhamu

WATUMISHI watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na matumizi mabaya ya fedha za makusanya ya mapato ya ndani na kushindwa kuwasilisha serikalini.

Pia, watumishi wengine wameshushwa vyeo, kusitishiwa mikataba ya ajira na kusimamishwa kazi kwa ajili ya uchunguzi.

Akitoa taarifa ya uamuzi huo mbele ya wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Peter Nzalalila, alisema watumishi hao wamefukuzwa na wengine kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka maadili ya utumishi wa umma pamoja na misingi ya utawala bora.

Alisema uamuzi huo umefanywa kutokana na mapendekezo ya kikao cha Kamati ya Fedha, Mipango na Uongozi kilichoketi Mei 18, 2020 na kujadili tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi hao na hatua zinazostahili kuchukuliwa baada ya kuitwa na kuhojiwa.

Aliwataja waliofukuzwa kuwa ni Jacob Chapaulinge (Mtendaji wa Kata), Donald Lyoba (Mtendaji wa Kijiji) na Elia Kaugila (Mtendaji wa Kijiji), huku Sabina Mhaya (Mtendaji Kata ya Ngoywa) akipewa onyo na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi sita na kukatwa asilimia 15 ya mshahara kwa kipindi cha miaka mitatu.

Nzalalila alibainisha watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu kwa kusitishiwa mikataba yao ya ajira kuwa ni Simon Michael Nonga, Rashid Bakari Namalembo, Charles Henry Kaswiza, Mipawa Jilala Kamuga na Nigangwa Baruga wote walikuwa madereva.

Alitaja watumishi waliovuliwa madaraka ya ukuu wa shule kwa tuhuma za kushindwa kusimamia miradi katika maeneo yao kuwa ni Baraka Lyandala aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majojoro na Mandi Nghulingi, aliyekuwa Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kiloleni.

Vile vile, Mapambano Masota alivuliwa nafasi ya Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilumbi, Mtendaji wa Kijiji cha Kiyombo, Wistone Ikanga, alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi, huku Ofisa Elimu Msingi wa wilaya hiyo, Suzana Makoye na Ofisa Elimu Kata ya Kilumbi, Magesa Keneja wakipewa onyo la kwanza.

Akizungumza na gazeti hili, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tito Luchagula, alisema adhabu hizo ni sahihi kwa kuwa watumishi hao walienda kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwamo vitendo vya utovu wa nidhamu na ubadhirifu.

Habari Kubwa