Watumishi wawasilisha hoja tisa za kudai haki serikalini

26Jan 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Watumishi wawasilisha hoja tisa za kudai haki serikalini

CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), kimewasilisha kwa serikali hoja tisa ambazo zimekuwa kikwazo kwa watumishi wa elimu ya juu nchini, huku kikitoa mapendekezo mbalimbali.

Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu sura ya 178 ambayo ni tatizo katika ukusanyaji na urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika.

Akizungumzia hoja hizo zilizowasilishwa kwa Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie, alisema kumewapo na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi kuhusu kubambikiwa madeni wasiyostahili kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo.

Alisema katika sheria hiyo ya bodi kuna sharti la kuanza kulipa deni baada ya zaidi ya miaka miwili baada ya kumaliza au kusitisha masomo hali inayosababisha wanufaika kuandamwa na malipo ya adhabu mbali na asilimia 15 ya makato ya mshahara wakati wa marejesho yao.

“Mwanzoni sheria iliweka angalizo kuwa makato ya mkopo kwenye mshahara wa mfanyakazi mnufaika yasizidi theluthi moja ya mshahara, lakini marekebisho haya hayajazingatia umuhimu huu wa kiwango cha makato na kushusha morali ya kufanya kazi,” alisema.

Hata hivyo, alisema utaratibu ulioanzishwa na Bodi hiyo wa tozo ya kutunza thamani (VRF) umeonyesha mdaiwa atalazimika kulipa deni kwa muda mrefu na kushindwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Alisema chama hicho kinashauri serikali kufanyia marekebisho mbalimbali sheria hiyo ikiwamo kupunguza makato ya asilimia 15 ili kuwapunguzia machungu wafanyakazi.

MASLAHI YA WAFANYAKAZI

Alisema licha ya serikali kulifanyia kazi kwa kiwango kikubwa suala la malimbikizo ya mishahara, lakini bado wafanyakazi wana madai mengi.

“Tunashauri serikali kuendelea kujipanga kulipa madeni yote halali yanayowasilishwa na vyuo vijitahidi kuzuia madeni mapya kuzalishwa,” alisema.

UPANDISHAJI VYEO

Dk. Loisulie alisema kumekuwapo na mkanganyiko usio wa lazima katika utekelezaji wa nyaraka za upandishaji vyeo hali inayosababisha kuchelewa kupata mishahara mipya inayoendana na vyeo vyao.

“Tunashauri Ofisi ya Rais, Utumishi iendelee kutoa nyaraka za kutoa ufafanuzi kwenye taasisi za umma ili kuepuka tafsiri tofauti kwa taasisi moja hadi nyingine,” alisema.

MABADILIKO YA SHERIA YA UTUMISHI

Alisema marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma namba nane ya mwaka 2002 yaliyofanywa mwaka 2016 yamesababisha kero kubwa kwa watumishi hasa utaratibu wa kushughulikia masuala ya kinidhamu katika utumishi wa umma.

Alisema THTU inashauri serikali kuifanyia marekebisho sheria katika Sura ya 298 kwa kuondoa sharti la lazima kwa mtumishi wa umma kumaliza kwanza nafuu zote za kisheria zinazoainishwa kwenye sheria ya utumishi wa umma kabla ya kutafuta nafuu za kisheria kwenye sheria ya kazi.

BIMA YA AFYA

Alisema hivi karibuni kumetokea mabadiliko katika utoaji wa huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hali ambayo inaathiri wafanyakazi wote nchini ikiwamo mabadiliko ya wategemezi.

“Kumwondoa mtoto ambaye ametimiza miaka 18 kwenye utegemezi licha ya kuwa bado yupo chini ya wazazi, kwa mazingira ya kitanzania watoto hawa bado ni wategemezi kwa kuwa wapo masomoni, hii hali imeongeza mzigo kwa wazazi kulipa Sh. 50,400 anapokwenda chuoni,” alisema.

Alishauri mfuko huo kuruhusu utaratibu uliokuwapo awali wa kuendelea kuwepo kwa wategemezi vijana hao hadi atakapofikisha miaka 26.

Pia, alishauri endapo kuna utofauti wa kadi na huduma zinazotolewa mfuko unatakiwa kuwa wazi ili kutoibua malalamiko.

MABORESHO YA MIUNDO YA UTUMISHI

Alisema THTU inaamini kuwapo kwa miundo inayofanana ya taasisi hizo kutapunguza kila taasisi kuwa na muundo wake na kupunguza kuhama kwa sababu za mishahara.

UTAWALA BORA

Alisema baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wamekuwa wakikiuka misingi ya utawala bora kwa sababu zisizoeleweka ikiwamo kuficha nyaraka zinazotoka serikalini zinazohusu maslahi ya wafanyakazi.

Aliomba serikali kuzielekeza menejimenti za taasisi za elimu ya juu kuzingatia miiko ya utawala bora wakati wa utekelezaji wa mamlaka yao.

KILIO VYUO BINAFSI

Dk. Loisulie alisema wafanyakazi waliopo vyuo binafsi wanakabiliwa na tatizo la kutolipwa mishahara kwa wakati, waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na bodi ya mikopo.

“Tunashauri serikali kuzihamasisha na kushauri taasisi binafsi za elimu ya juu kubuni vitega uchumi vya kuongeza pato la taasisi ili kuepukana na kushindwa  kulipa mishahara ya wafanyakazi,” alisema.

Alisema wanaamini serikali itachukua hoja hizo na kuzitafutia ufumbuzi ili kuwa na tija kwa wafanyakazi.

Habari Kubwa