Wauawa madai mgogoro shamba

16Oct 2020
Frank Kaundula
Morogoro
Nipashe
Wauawa madai mgogoro shamba

WATU wawili wameuawa kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Mafisa kwa Mambi, Manispaa ya Morogoro huku chanzo cha mauaji hayo kikidaiwa mgogoro wa shamba.

Mauaji ya watu hao yalitokea usiku wa kuamkia jana yakidaiwa kuwa yametokana na mgogoro wa shamba katika kijiji cha Kisaki wilayani Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa tayari jeshi hilo linamshikilia Rajabu Hamisi (26) mkazi wa Msamvu Ndege Wengi, Manispaa ya Morogoro.

“Ni kweli tukio hilo lipo na huyo mtuhumiwa tumeshamkamata na tunaendelea kumhoji. Upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Mutafungwa.  

Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Bernadetha Kibwana anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 60 na 665 mkazi wa kijji cha Kisaki, ambaye inadaiwa alikuwa ndiye mlengwa katika tukio hilo na Zaibabu Maulid mkazi wa Mafisa kwa Mambi, ambaye anadaiwa alikuwa akijaribu kutoa msaada.

Kamanda alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwa Martha Mkude, ambako alikuwa akiishi kwa muda na Kibwana,  ambaye inadaiwa alikuwa akisubiria kesi yake ya shamba katika Mahakama ya Ardhi. Kesi hiyo ilipangwa kutajwa Oktoba 29, mwaka huu.

Mkude, mmliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Kibwana, alisema watu wasiojulikana walianza kuvamia nyumba za jirani kwa lengo la kumtafuta bibi huyo na walipofika katika chumba alichukuwa amelala, walianza kumshambulia.

Alisema baada ya watu hao kufanikisha mauaji ya mama huyo ndipo alipojitokeza jirani yake, Maulidi kwa lengo la kumsaidia, bila mafanikio kisha naye kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Naye Athumani Bakari, ni mjukuu wa Kibwana, alisema bibi yake alikuja mjini kwa lengo la kumtibia mjukuu wake mwingine, ambaye ni mlemavu wa viungo baada ya kupigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni msamaria mwema anataka kuwasaidia.

Alisema baada ya kufika, bibi huyo alianza kumtilia shaka msamaria huyo kutokana maswali yake, ndipo alipoamua kumpigia simu mjukuu wake kuondoka na kwenda nyumbani na Martha kwa ajili ya kusubiria kesi yake.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mafisa kwa Mambi, Ahmed Salum, alisema baada ya kupata taarifa kwa majirani kuhusu tukio hilo, alifikisha taarifa polisi na kwamba hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwamo kumkamata mtuhumiwa.

Habari Kubwa