Wauguzi wakumbushwa wajibu

16Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wauguzi wakumbushwa wajibu

MHADHIRI Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha St. John’s kilichopo Dodoma, Faraja Mpemba, amewakumbusha wauguzi kuwa wanaowahudumia hospitalini ni wateja wao hivyo wanatakiwa kutumia lugha nzuri.

WAUGUZI.

Mpemba aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika maonyesho ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na kushirikisha vyuo mbalimbali nchini.

Akizungumzia kuhusu lugha zinazotakiwa kutolewa kwa wagonjwa, Mpemba alisema wanapotoa mafunzo vyuoni huwafundisha wanafunzi kuwa wanaowahudumia siyo wagonjwa bali wateja.

“Tunawaita wateja kwa sababu ndiyo wanaotufanya tuwepo kazini, unapomuhudumia mteja wako unatakiwa uwe na lugha ambayo itamfanya siku nyingine akiwa na shida arudi kwako,” alisema.

Mpemba alitoa wito kwa watoa huduma za afya wakiwamo wauguzi kuhakikisha wanatumia elimu walizopata vyuoni kuwahudumia wateja wao vizuri.

“Hata kama mtu utakuwa na matatizo tofauti nyumbani ukifika kazini unayaacha huko na kuwahudumia wateja vizuri,” alisema.

Alisema mbali na masomo mengine wanayotoa chuoni hapo pia wanawafundisha wanafunzi namna bora ya kuwahudumia wateja na kuwa wa wamawasiliano mazuri.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Prof. Timothy Simalenga, alisema chuo hicho kinatoa shahada mbalimbali mikondo kama sita na masomo yasiyo ya shahada mikondo kama 16.

Pia alisema chuo chao kinafundisha somo la Kiswahili na kimekuwa kikiunda maneno ya Kiswahili na kuwezesha kutunga sentensi mbalimbali.