Waumini waandamana kushinikiza askofu wao kurejeshwa

29Nov 2021
Elizabeth John
NJOMBE
Nipashe
Waumini waandamana kushinikiza askofu wao kurejeshwa

BAADHI ya waumini wa Kanisa la Makambako Christian Center (MCC) lililopo Halmashauri ya Mji Makambako Mkoa wa Njombe wamelazimika kuahirisha ratiba zote za ibada na kufanya maandamano kushinikiza kurejeshwa kwa mchungaji wao-

-wanaedai kuondolewa kanisani hapo na Mwenyekiti wa Ushirika wa Makanisa Tanzania (TFC), Askofu Godfrey Malasi bila kufuata katiba ya kanisa hilo.

Wakizungumza na Nipashe Digital waumini hao wameiomba serikali kuingilia kati ili kumaliza mgogoro huo huku wakieleza nia yao ni kuachana na ushirika huo pamoja na kurejeshewa mchungaji wao jambo ambalo mwenyekiti wa TFC anadaiwa kushindwa kulitekeleza.

"Mgogoro huu umesababishwa na mwenyekiti wetu ambaye anajiita askofu ni mtu ambaye hapendi kushirikiana uongozi wa kanisa au waumini kwenye maamuzi hasa ili la kumtoa mchungaji,hatuwezi kuendelea nae kwa sababu licha ya kumlalamikia kwa barua kadhaa lakini anatupuuza" amesema Musa Kambo. 

Naye Ester Jeremia amesema kuwa wao waumini hawana mgogoro na mchungaji wao isipokua mwenyekiti huyo ndio anakiuka katiba.

Alijibu malalamiko hayo  kwa njia ya simu, Askofu Malasi amesema mgogoro huo ni wa muda mrefu.

"Limeshughulikiwa hapa sio leo tu linamlolongo mrefu tangu mwezi wa saba,utaratibu mbalimbali umefanyika ila kwa sababu ni watu wa fujo walikua wanasimamiwa na vyombo vya usalama"amesema Askofu Malasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah amefika kanisani hapo na kutoa wito kwa taasisi na vikundi kuwa na uwazi katika mifumo ya uendeshaji wa taasisi zao ikiwa ni pamoja na kuweka bayana taratibu walizojiwekea.

"Kwa hali kama hii na waumini walivyokua wengi,tumekuta kuna mabango yapatayo 40 na yote yakiwa yanapinga uamuzi wa askofu" amesema Kamanda Issah

Habari Kubwa