Waumini watahadharishwa kutoa sadaka noti bandia

21Jan 2019
Marco Maduhu
 SHINYANGA
Nipashe
Waumini watahadharishwa kutoa sadaka noti bandia

WAUMINI wa Kanisa la Advestista Wasabato Shinyanga Mjini, wametakiwa wawe wanazikagua fedha zao ambazo huzitoa sadaka  ili kuepuka kumtolea Mungu fedha haramu za noti bandia.

kapu la sadaka.

Wito huo ulitolewa na mweka hazina  wa kanisa hilo, Amosi Magige, wakati wa matangazo ya kanisa, kuwa wiki iliyopita alipokuwa akipeleka fedha za sadaka benki, alikumbana na changamoto ya kuwapo na noti bandia ya Shilingi 10,000.

Alisema wakati akiweka fedha hizo benki, ghafla aliambiwa kuwa katika fedha zake hizo kuna pesa bandia noti ya Shilingi 10,000 kitendo ambacho kilimtia wasiwasi kuwa huenda labda ataitiwa polisi na kutiwa nguvuni.

“Napenda kutoa tahadhari kwenu waumini wa kanisa hili, pale mnapokuwa mnaleta pesa za sadaka jaribuni kuwa mnazichunguza kwanza kama siyo noti bandia, ili kutuepusha kuingia matatizoni na kama pesa hizi zisingekuwa ni za kanisa sijui ingekuwaje,” alisema Magige.

“Baada ya kuambiwa katika fedha za sadaka kuna noti bandia kijasho kilianza kunitoka nikajua basi nimekwisha, lakini mfanyakazi huyo wa benki akaishia kusema tu na huko napo zipo hizi, basi ndio ikawa pona yangu na kuamua kutoa pesa nyingine ili kujazilizia, ambazo zilikuwa za michango mingine,” aliongeza.

Aidha, alisema kwa muumini ambaye hazifahamu noti bandia anaweza kumuona baadaye baada ya ibada kuisha.

Waumini waliitikia wito huo, huku wengine wakidai kuwa hawazijui noti bandia, na kueleza kuwa siyo rahisi mtu kwenda kumtolea Mungu sadaka fedha bandia kwa makusudi bali inahitajika  elimu ya kuzitambua.

Habari Kubwa