Wauzaji viumbepori wamwangukia JPM

19Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wauzaji viumbepori wamwangukia JPM

WASAFIRISHAJI nje ya nchi viumbepori hai wamemwomba Rais John Magufuli awasaidie ili biashara hiyo iliyositishwa miaka mitatu iliyopita, irejee kwa sababu hawasafirishi wanyama bali viumbepori.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama cha Wasafirishaji Viumbepori Hai Nje ya Nchi (TWEA), Adam Waryoba, alisema mwaka 2016 serikali ilisitisha ghafla ukamataji na usafirishaji nje ya nchi viumbe hao.

Alisema wakati wa tamko hilo lililotolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, walikuwa tayari wameshalipa serikalini vibali vya usafirishaji.

“Miaka mitatu ya sitisho imeisha Machi 16, mwaka huu, mchakato wa biashara kwa mwaka unaofuata huanza Oktoba na Novemba mwaka uliotanguli, lakini wizara kupitia Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa) Februari Mosi, mwaka huu, ilitangaza leseni za biashara za mwaka huu, bila kutangaza leseni tunazofanyia biashara,” alisema.

Alisema wizara haijatamka lolote kuhusu wao kuanza biashara hiyo baada ya kipindi cha sitisho kuisha.

“Waziri wa sasa wa wizara hiyo, Dk. Hamis Kigwangalla, Mei 21, mwaka jana, alilieleza Bunge kuwa serikali itaturudishia Sh. milioni 173.3 tulizo lipa lakini hadi sasa hawajafanya hivyo na hatujajua hatima ni nini,” alisema Waryoba.

Alisema biashara hiyo wanayoifanya inawahusu viumbepori hai ambao ni vyura, wadudu, mijusi, ndege na tumbili.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, baada ya kuilipa serikali fedha hizo, waliendelea na shughuli za ukamataji wa viumbepori hai na wakati sitisho hilo linatoka, walikuwa kwenye maandalizi ya kusafirisha.

“Ndiio maana tunamuomba Rais Magufuli atusaidie kwa sababu fedha tumelipa, viumbepori tulikamata, leseni zetu zilizotoka kabla ya kusitishwa biashara hii zilikuwa 454. Tunamwomba Rais atusaidie tuendelee na biashara hii kuliko kuendelea kupata hasara na tuko tayari kukutana naye,” alisema.

Alisema biashara ya viumbepori hai ilianza kabla ya uhuru ambapo ilifanywa na wazungu kwa wanyama.

“Baada ya uhuru iliainishwa vyema kwa sharia ya uhifadhi wanyamapori ya mwaka 1974 na kufanywa kuwa ya Watanzania wazawa,” alisema.

Waryoba alisema mwaka 2012 leseni za wanyama ziliondolewa kwenye biashara kwa kuwa wanapatikana kwenye hifadhi ambako utalii unafanyika.

Alisema serikali ilibakiza leseni za vyura, wadudu, mijusi, nyoka, ndege, tumbili na nyani.

“Mgawo wa biashara ya viumbepori vyote ni kwa aina zile zilizopatikana maeneo ya wazi ambako wananchi wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi.

Alisema tangu wakati huo hadi sasa ukamataji wa viumbepori hai inafanyika kwenye mikoa isiyozidi minane kati ya 31 iliyopo ambapo ni sawa na asilimia 26.

Mfanyabiashara wa viumbepori hai, Deodata Nsimeta, alisema sitisho hilo limemwathiri kwa sababu alikopa fedha, alikusanya viumbepori ambao waziri aliwaeleza watakwenda kuwachukua lakini hadi sasa hawajafanya hivyo.

Habari Kubwa