Wavuvi walia na kanuni za uvuvi

13Aug 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wavuvi walia na kanuni za uvuvi

WAVUVI wa Soko la Samaki la Kimataifa Feri jijini Dar es Salaam, wamepinga kanuni za uvuvi ya mwaka 2020 wakidai siyo rafiki kwao na adhabu zake hazitekelezeki.

Waliwasilisha kilio chao hicho kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza sokoni huko na kufanya kikao nao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya waziri huyo, wavuvi hao walisema kanuni hizo siyo rafiki kwao na hazikuzingatia mapendekezo waliyoyatoa awali.

Mratibu wa Vyama vya Sekta ya Uvuvi Ukanda wa Pwani, Mohamed Muhidini, alimwambia waziri huyo kuwa, kanuni za mwaka 2020 siyo rafiki kwao, hivyo waliamua kusitisha shughuli za uvuvi baharini kwa muda.

“Kanuni zilizopo siyo rafiki kwetu, hukumu zake ni ngumu, hazitekelezeki na zina mengi ambayo mpaka unakuja hapa ni kwamba mmeshayapitia.

“Faini zilizopo siyo rafiki, maelekezo kuhusu matumizi ya zana za uvuvi yanakanganya, maeneo ya kazi tuliyoelekezwa na kanuni siyo rafiki, unapomwambia mtu avue mita 50 kwa ekolojia ya hapa ni bahari kuu ambapo vyombo vyetu havina uwezo huo," alilalamika.

Faki Faki, mmoja wa wavuvi hao alisema kuwa Oktoba walikutana Dodoma kwa ajili ya kutoa maoni yao ili kuboresha kanuni hizo, lakini hayakuzingatiwa.

“Tulichangia, tukazindua rasimu ya kanuni ukumbi wa Karimjee, tukatoa maoni, bahati nzuri Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoad Mgimwa, alituambia 'ikiwa maoni yenu hayapo niambieni'.

“Nilikuuliza waziri umeleta hii rasimu isije ikawa umeshaipitia hii kusema toeni maoni ni kizungumkuti kumbe ndiyo jibu langu, hongera kwa hilo," alisema.

Akizungumzia kanuni hizo, Waziri Mpina alisema awali alitangaza kuwa atafumua Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 kwa sababu teknolojia na mazingira ya uvuvi yamebadilika.

Alisema aliona zifumuliwe ili kuweka mazingira bora kwa ajili ya wavuvi kwa sababu shabaha ya serikali siyo kuwakwaza wavuvi.

“Kulikuwa na mambo kama tozo zilikuwa kubwa, leseni nayo gharama zilikuwa kubwa, mwanzo kanuni ya tozo ya samaki mfano dagaa wa bahari ilikuwa kuwauza nje ya nchi ni dola moja na wa Ziwa Tanganyika dola 1.5.

“Nimepunguza kutoka dola moja hadi dola 0.3, mkasema hata hiyo hamtauza, imeshuka zaidi hadi dola 0.16, leseni ya kuuza mazao ya uvuvi, mvuvi wa dagaa anapotaka leseni ili kuyasafirisha kuuza nje ya nchi ilikuwa dola 1,000 na sasa ni dola 250, hili ni punguzo la asilimia 75," alibainisha.

Alisema mazao mengine kama kamba miti leseni ilikuwa dola 2,500 na sasa ni dola 500 wakati wafanyabiashara wa kaa ilikuwa dola 2,500 na kwa sasa ni dola 500.

Mpina pia alisema serikali imeamua kuanzia sasa leseni itakuwa ni moja na itatambulika kama leseni ya kuvua Bahari ya Hindi au ukanda wa Pwani kulingana na eneo.

“Ilikuwa ikifika Januari Mosi ulikuwa huruhusiwi kuingia majini mpaka ukate leseni, tumerekebisha hakuna mtu atakayemkamata mvuvi, mtakata polepole kwa miezi mitatu mpaka Machi,” alisema.

Waziri huo alisema soko hilo kila mwezi linakusanya Sh. milioni 100 ambazo zilikuwa zikitumika kwa matumizi ya kawaida, lakini kwa sasa wanabakiza Sh. milioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu.

“Vyoo vilikuwa vilevile, vimejengwa, majengo yamejengwa, tulikuta watu wanaweka samaki kwenye mchanga na sasa yapo maeneo na ukarabati bado unaendelea,” alisema.

Mpina alisema kwa sasa wako kwenye hatua ya mwisho ya utoaji wa Sh. bilioni 1.7 ambazo zitatumika kukarabati miundombinu sokoni hapo.

Awali, Katibu Tawala Wilaya ya Ilala, Charangwa Seleman, alisema tatizo kubwa ambalo wavuvi wamemweleza ni kanuni mpya zinazozuia kuvua mchana na walishapeleka malalamiko hayo maeneo mbalimbali.

Habari Kubwa