Wawanyanyapa wagonjwa wa TB kwa kuogopa kuambukizwa corona

25Mar 2020
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Wawanyanyapa wagonjwa wa TB kwa kuogopa kuambukizwa corona

Wananchi wa mikoa ya Shinyanga na Geita wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kuwanyanyapaa na kuwanyima chakula wagonjwa wa kifua kikuu (TB) na Ukimwi kwa kisingizio kuwa wanaweza kuwaambukiza virusi vya ugonjwa wa corona.

Kaimu Mkurugenzi wa miradi Shekha Nassoro kutoka shirika lisilo la kiserikali la Shdepha+ jana katikati akiwaweleza wanahabari hawapo pichani namna wanavyotoa elimu ya TB baada ya ugonjwa wa Corona kuingia nchini (PICHA NA SHABAN NJIA)

Ofisa wa mradi wa Kifua Kikuu kutoka Shirika lisilo la kiserikali SHDEPHA+ Wilaya ya Kahama, Anasia Mringo, amesema kwa sasa ongezeko la unyanyapaa kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu na Ukimwi katika mikoa ya shinyanga na Geita umeongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma na hiyo inatokana na kuwepo kwa taharuki ya ugonjwa wa corona hapa nchini.

Mringo ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni moja ya shughuli za maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu ambayo hufanyika kila mwaka Machi 24.

Amesema kuwa kwasasa wagonjwa wa TB wananyanyaswa na kunyanyapaliwa kwa kunyimwa chakula kwa madai wanapowasogelea wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa corona, kutokana na ugongwa huo uambukizwa kwa njia ya hewa kama ilivyokwa virusi vya corona.

“Mgonjwa wa TB anapoanza kutumia dawa hawezi kumuambukiza mtu anaishi nae, anaponyimwa chakula afya yake hudhoofika sana…..kunyanyapaliwa kwa wagonjwa wa TB na Ukimwi imetokana na virusi vya ugonjwa wa corona vilivyoingia hivi karibuni” amesema Mringo.

Meneja mradi wa kifua kikuu Mwinuka Ereneus na Mratibu uhakiki na tathimini Rabia Abeid kutoka Shdepha+ jana wakiwa wameshika bado lenye maneno LINDA AFYA YA MAPAFU YAKO DHIDI YA KIFUA KIKUU kama moja ya maadhimishi ya siku ya kifua kikuu Duniani. PICHA: NA SHABAN NJIA

Aidha Mringo amesema wachimbaji wadogo nao wako hatarini kukumbwa na janga la virusi vya corona na TB,hivyo ili kudhibiti janga hilo wameanza kutoa elimu ya kujikinga na virusi hivyo na TB kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu kupitia kwa watoa huduma ngazi za kata na vijiji.

Kwa upande wa Mratibu Uhakiki na Tathimini, Rabia Abeid, amesema kuwa,changamoto wanazokutana nazo wakati wa utoaji elimu juu ya kujikinga na TB ni wananchi kushindwa kutoa makohozi yao kwa ajili ya vipimo kwa madai ya kuhofia wanakwenda kurogwa au kuwa na imani ya wanaopima ni freemasoni.

Meneja Mradi wa Kifua Kikuu, Mwinuka Ereneus, amesema kuwa, mradi wa TB unatekelezwa katika Mikoa ya Geita na Shinyanga katika Halmashauri nne za Mbogwe, Masumbwe, Kahama mjini pamoja na Halmashauri ya Msalala.

Hata hivyo amewataka wananchi wa mikoa hiyo kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujikinga na ugonjwa wa kifua kukuu,Ukimwi na corona kutokana na magonjwa hayo mengi huambukizwa kwa njia ya hewa ukiachilia ukimwi.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Miradi, Shekha Nassoro amesema kuwa, kwasasa wamesitisha utoaji wa huduma kwa kuwafuata wagonjwa majumbani na sehemu za wachimbaji wadogo kutokana na corona na badala yake wanatoa elimu ya kujikinga kwa njia ya ujumbe wa simu.

 

 

Habari Kubwa