Wawaozesha watoto wao wadogo kwa pombe

08Dec 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Wawaozesha watoto wao wadogo kwa pombe

WANANCHI wa kijiji cha penzi kata ya Mondo katika Halmashauri ya mji wa Kahama Mkoani Shinyanga, wamesema kuwa, ongezeko la mimba kwa watoto wadogo wa kike na ukatili wa kijinsi dhidi yao unasababishwa na wazazi kuwaozesha kwa jagi moja ya pombe virabuni.

Hayo waliyabainisha jana kwenye Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto,yaliyofanyika katika kijiji cha penzi kata ya mondo kupitia Shirika lisilo la kiserikali la World Vision chini ya mradi wa Enrich.

 Angelina Sulemani ni mkazi ​​wa kijiji hicho alisema kuwa,akinababa wamekuwa wakiwaozesha watoto wao wa kike bila kuwajulisha kwa kubadilishana na jagi moja ya pombe wawapo virabuni au mifugo aina ya ng’ombe. 

Alisema kuwa kulingana na mila na desturi za Kisukumu hawaruhusiwi kuhoji inabidi wakubali mwanawe aolewa japo anasoma na makubaliano yanakuwa yamefanyika kwenye virabu wakati wanakunywa pombe na wanapokataa wanaambulia kipigo.

Kwa upande wa q Malia Emmanuel alisema kuwa,wakati mwingine unakuta mtoto anafanya vizuri kwenye masomo yake lakini baba yake anamtaka kufanya vibaya kwenye mitihani yake kwa kisingizio hala fedha ya kumsomesha na unapofuatilia unakuta ameshakula mahali.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale alisema,ili kukomesha vitendo hivyo,wameanzisha utaribu wa mtoto wa kike anaefanya vizuri kwenye masomo,mzazi anatakiwa kufunga mkataba na mwalimu mkuu wa shule anayosomea na atakapofanya vibaya mzazi atawaajibika kisheria.

Pia Ngwale alisema,hakuna ndoa yoyote itakayofungwa kuanzia ngazi ya kijiji,kata hadi wilaya bila yakuwa na cheti cha kuzaliwa ambacho kitaonesha umri wa anakwenda kuolewa na akiwa chini ya miaka 18 wazazi wa pande mbili watashitakiwa.

“Kwasasa mmebinu mbinu mpya ya kuwaozesha watoto wenu,mnamuozesha binti mwenye umri wa kuolewa mchana na usiku ukifika mnampleka mtoto wenu kwa mlengwa,hii mbinu tunaifahamu na tunaifuatilia na lazima tuwabaini na kuwafungulia mashitaka"alisemaNgwale.

Aidha Ofisa Jinsia na utetezi wa mradi wa Enrich kutoka shirika la World Vision Magreth Mambali alisema,wamekuwa wakitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili ikitokea ukatili watambue wapi wanatakiwa kwenda kupata msaada.

Hata hivyo alisema kuwa,waendesha baskeli na bodabonda wamekuwa chanzo kikubwa cha kusababisha mimba za utotoni kwa watoto wakike na kutoa wito kwa wadau na serikali kusogeza huduma za kishule hasa elimu ya sekondari karibu na makazi ya watu.

Habari Kubwa