Wawekezaji Syria wavutiwa kuwekeza Tanzania

20Mar 2019
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Wawekezaji Syria wavutiwa kuwekeza Tanzania

MAMLAKA ya Ukanda Maalum ya Uwekezani nchini (EPZA), imesema wafanyabiashara na wawekezaji wanaoshiriki maonyesho ya kimataifa ya Syria wameonyesha kuvutiwa na fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Uhamasishaji Uwekezaji wa EPZA, Grace Lemunge, katika maonyesho ya kimataifa ya Syria yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

“Wawakilishi wa kampuni zinazoshiriki katika maonyesho ya kimataifa ya Syria waliotembelea banda la EPZA, wamevutiwa sana na fursa za uwekezaji hasa kwenye viwanda kupitia mamlaka ya EPZA,” alisema.

Alisema lengo la EPZA kushiriki maonyesho haya ni kuwafungulia milango na kuwapa taarifa sahihi zihusuzo fursa za uwekezaji katika viwanda washiriki wa maonyesho hayo.

Lemunge alisema wafanyabiashara na wawekezaji wameahidi kupeleka taarifa hizo muhimu za fursa za uwekezaji zilizoko Tanzania katika nchi zao ili kuwashawishi wawekezaji wengi zaidi kuja nchini.

Alisema uwekezaji kupitia maeneo hayo ya ukanda maalum wa uwekezaji (SEZ), mwekezaji hupata fursa ya soko kubwa la ndani na nje, unafuu mkubwa katika kodi na wafanyakazi wa kutosha.

“Kupitia EPZA kuna fursa za kuwekeza kupitia kwenye maeneo ya ukanda maalum (SEZ). Asilimia 80 ya bidhaa zinazozalishwa huuzwa nje ya nchi na kiwango kilichobaki huuzwa nchini,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi Uhamasishaji wa EPZA, Panduka Yonazi, alisema maonyesho kimataifa ya Syria yanayoendelea yamekuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Syria na nchi zinigine za Asia kupata taarifa muhimu za uwekezaji katika viwanda nchini.

Alisema pia wafanyabiashara na wawekezaji wazawa nao pia wamekuwa mstari wa mbele katika kupata taarifa za fursa mbalimbali zinazotangazwa katika banda la mamlaka ya EPZA yanapofanyika maonyesho hayo.

“Wafanyabiashara wazawa ambao wanashiriki katika maonyesho ya kimataifa ya Syria wamekuja kwa wingi sana katika banda la EPZA ili kupata taarifa juu ya fursa za uwekezaji katika viwanda nchini,” aliongeza kusema.

Yonazi alisema EPZA inawahimiza washiriki wa maonyesho hayo wanaotoka nje ya Tanzania kupata maelezo ya kina juu ya uwekezaji na kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana.

Habari Kubwa