Wawili mbaroni kwa kukutwa na nyara za serikali, bangi

28Nov 2021
Neema Hussein
Katavi
Nipashe Jumapili
Wawili mbaroni kwa kukutwa na nyara za serikali, bangi

JESHI la polisi mkoani Katavi, linamshikilia Seda Mbutula (47) kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali zidhaniwazo kuwa ni mafuta ya simba, ngozi ya kakakuona, ngozi ya paka pori vipande vinne vya meno ya ngiri na mkia mmoja wa nyumbu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Ali Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Ali Hamad, ambapo amesema tukio hilo limetokea Novemba 23 mwaka huu katika pori la akiba Rungwa lililopo Kata ya Ilunde Wilaya ya Mlele mkoani humo.

Hamad amesema baada ya oparesheni maalumu walifanikiwa kumkamata mtu huyo akiwa amehifadhi nyara hizo kwenye mfuko wa salfeti na kuficha ndani ya nyumba yake.

Sambamba na hilo pia Jeshi la Polisi limemkamata Samweli Kazambi (36) kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni bangi.

Kamanda Hamad amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 24 mwaka huu katika kijiji cha Milala Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi akiwa na bangi jumla ya kete 12 na mbegu za bangi zenye uzito wa gramu 1000 ambazo alihifadhi ndani ya nyumba yake.

Hata hivyo kamanda Hamad amesema sambamba na mafanikio hayo, Jeshi la Polisi katika Mkoa huo linaendelea kuwasisitiza wananchi wa Katavi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuendelea kuzisalimisha hasa kwa kipindi hichi cha msamaha uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Amesema zoezi hilo lilianza Novemba 11 na linatarajiwa kumalizika Novemba 30 mwaka huu kwa wale wote watakao zisalimisha silaha zao ndani ya muda huo watapewa msamaha wakutokushitakiwa.

Aidha, amewataka wananchi wote wa Mkoa huo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kihalifu na wahalifu ili kuendelea kuuweka Mkoa huo katika hali ya usalama.

Habari Kubwa