Wawili wafa ajali ya basi na bajaji

26Mar 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wawili wafa ajali ya basi na bajaji

WATU wawili wamepoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Ifakara mkoani Morogoro lililogongana uso kwa uso na bajaji eneo la Ilomba jijini Mbeya.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, picha mtandao

Akizungumza na wandishi wa habari jijini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alilitaja gari lililohusika kwenye ajali hiyo kuwa ni lenye namba za usajili T 413 AVU, mali ya Kampuni ya Rahabu ambalo liligongana na bajaji yenye namba za usajili MC 230 BGT aina ya TVS.

Alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:15 asubuhi wakati mabasi yalipokuwa yanaanza safari zake kutoka jijini Mbeya kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Aliwataja waliofariki dunia kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa bajaji ambaye jina lake bado halijafahamika pamoja na abiria wake, Ester Mbonje (35), mkazi wa Ilemi jijini Mbeya.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi kuendesha gari bila kuwa makini kwa kutaka kulipita gari lingine bila kuangalia mbele na hivyo kukutana na bajaji uso kwa uso na kupelekea bajaji hiyo kupinduka.

“Baada ya kugongana, bajaji ilipinduka na kuwasababishia majeraha waliokuwa ndani yake, wawili hao walifariki dunia wakati wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya,” alisema.

Kamanda Matei alisema kuwa baada ya ajali hiyo kutokea, dereva wa basi, Ayoub Mwandwanga (36), ambaye ni mkazi wa Ilomba jijini Mbeya, alikamatwa na anaendelea kushikiliwa na polisi wakati akisubiria hatua zaidi za kisheria.

Alisema Jeshi la Polisi linaichukulia ajali hiyo kuwa ni ya makusudi kutokana na namna ambavyo dereva wa basi hilo alivyofanya kile alichokiita uzembe.

Aliwataka madereva wa vyombo vya moto mkoani humo kuwa makini kwa kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka kusababisha ajali ambazo hazina ulazima.

Kamanda Matei alisema miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye hospitali hiyo ya kanda, akiwataka wananchi kwenda kuutambua mwili wa dereva wa bajaji.

Habari Kubwa