Wawili wafa, sita wajeruhiwa ajalini

07Apr 2020
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Wawili wafa, sita wajeruhiwa ajalini

WATU wawili wamefariki dunia na wengine sita wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea juzi kwenye barabara ya Arusha- Namanga.

Kati ya waliyofariki katika ajali hiyo, ni Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Enock Wange (41), na Julius Saitoti.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Koka Moita, alisema ajali hiyo, ilitokea juzi majira ya jioni katika eneo la Landakarai Kijiji cha Ranch Kata ya Olbomba Tarafa ya Longido.

Aliwataja waliyojeruhiwa ni Azaeli Mbise (37), ambaye ni dereva wa gari, Lolubare Kilesi (44-50) ,Gasto Mushi (32), daktari wa Hospitali ya Longido, Saluni Lengireri (50), Kondo Kibwana na (60), Justine Lobikeki (24).

Moita alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari namba T.742DGP Toyota PSV Noah, mali ya Ndete Lengai kupasuka gurudumu la nyuma upande wa kulia na kuacha njia.

Hata hivyo, alisema gari hilo, lilikuwa kwenye mwendokasi na lilimshinda dereva kulimudu.

Kamanda Moita alisema hali za majeruhi ni mbaya kwa kuwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili na wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) na ya Wilaya ya Longido.

Aidha, alisema miili ya waliokufa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufani ya Mount Meru.