Wazazi walezi wajikite malezi ya watoto miaka 0-8

08Dec 2023
Julieth Mkireri
KIBAHA
Nipashe
Wazazi walezi wajikite malezi ya watoto miaka 0-8

ILI kuwa na watoto wenye malezi bora, afya na ukuaji timilifu ni lazima Wazazi na Walezi kubadili mfumo wa malezi na kuwa karibu na watoto wao wakiwa bado na umri mdogo.

Kila mmoja ametakiwa kuzingatia jukumu lake katika malezi ya watoto kuanzia umri wa miaka  0-8 hususani katika lishe huduma za afya ujifunzaji wa awali na ulinzi kwa watoto ili wakue katika malezi bora kiakili na kimwili

Janet Christian, kutoka Taasisi ya Anjita  ambayo inafanya kazi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani alieleza hayo katika uzinduzi wa programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya awali ya mtoto katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Charles Lawiso amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la UNICEF inaonyesha Mkoa wa Pwani umefikia ukuaji timilifu  wa watoto kwa asilimia 48.8 katika masuala ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto.

Katika taarifa yake kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mshamu Munde alisema asilimia 51.2  ya watoto hawakuwa  katika ukuaji timilifu sababu ikiwa kutopata huduma Jumuishi zikiwemo afya bora, lishe elimu, Malezi yenye mwitikio na Ulinzi na usalama wa mtoto.

Alisema program hiyo  inakusudia kumkuza mtoto kimwili, kiakili, lugha, kijamii kitamaduni kihisia na kimaadili ambapo pia program hiyo ya MMMAM inalenga kutoa huduma za awali ulinzi na usalama kwa watoto.