Wazazi watakaochangia ukatili kwa watoto kuchukuliwa sheria

03Aug 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Wazazi watakaochangia ukatili kwa watoto kuchukuliwa sheria

Katika kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wazazi watakaochangia watoto wao kufanyiwa vitendo hivyo  ikiwemo mimba na ndoa za utotoni watachukuliwa hatua za kisheria.

Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solution on Gender Based Violence Anitha Samson akizungumza na Mwandishi wa habari hii.

Hayo yalibainishwa na Ofisa Elimu Taaluma Sekondari wa Manispaa ya Ilemela, Dorice Timotheo alisema Serikali kwa kushirikiana na mashirika binafsi yamekuwa wakiwahamasisha wazazi na walezi kupinga mimba na ndoa za utotoni kwa watoto wao ili kuwasaidia kutimiza malengo yao, lakini bado kuna baadhi yao wanachangia ongezeko la vitendo hivyo.

"Wapo wazazi ambao wamesha chukuliwa hatua  kuna watoto karibia 20 ambao walibeba mimba za utotoni kesi hizo zimekuwepo kwa mwaka 2019 hivyo wazazi wao wamechukuliwa hatua huku wengine wakichangia watoto kupatwa na ukatili hakika hatua kali zitachukulia dhidi ya mzazi hao " anasema Timotheo.

Hivyo aliwaomba wazazi kuwafatilia watoto wao hasa wa kike ili kuwasaidia watoto  kutimiza ndoto zao na kuepuka vitendo vya ukatili hususani wa kingono ambao  utakaoweza kuwasababishia magonjwa mbalimbali ya kingono vikiwemo Virusi vya Ukimwi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Ofisa Tarafa wa Ilemela, Godyfrey Mnzava anasema mbali na wazazi kuwa makini na watoto wao lakini pia walimu wanawajibu wa kuzungumza watoto hao pindi wawapo shuleni  kutoweka nafasi kati ya mtoto na mwalimu ili pindi mtoto anapokuwa na changamoto yoyote iwe rahisi kumuelezea mwalimu ili kulipatia ufumbuzi mapema na kama ni suala la kisheria walifikishe kwenye dawati la jinsia la polisi .

"Katika maeneo mengine mtoto wa kike anauwezo mkubwa kuliko hata wa kiume hivyo ni wajibu wa kumsaidia katika kutimiza ndoto zake kwa kumpatia elimu ya afya ya uzazi ambayo itamsaidia kujitambua na kujengewa uwezo wa yeye mwenyewe kusimama na kujitetea dhidi ya vitendo hivyo"anaeleza Mnzava.

Naye Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali linaloshughulika na kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto la WADADA Solution on Gender Based, Ruth John  anasema  kwa wakati huu tunahitaji wazazi kuwekeza zaidi kwa watoto ,kujenga urafiki na kuwapa elimu ya uzazi  na ukuwaji itakayowajengea uelewa na kuwa tija kwao.

Alisema kupitia mradi wa afya ya binti utasaidia Kuwafanya wazazi kutambua wajibu wao wa kuzungumza na watoto wao namna ya kujitambua na hatimae kuepuka kujihusisha na ndoa na mimba za utotoni.

Naye  Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Anitha Samson, wanaendelea na harakati za kupambana na changamoto zinazowakabili watoto hasa wa kike hivyo kupitia  mradi wa haki ya binti awamu ya pili unaotekelezwa katika Kata ya Kitangiri na Pansiasi  Wilayani humo ambao unalengo ya kuwafikia watoto wote hususani wa kike zaidi ya 400 ambao watapatiwa elimu mbalimbali kama stadi za maisha,ujasiriamali,elimu ya afya ya uzazi na uongozi bora ndani na nje ya shule.

Anasema mradi huo utakaohusisha wadau mbalimbali huku ukiwa na lengo la kuhakiksha mtoto wa kike anapata sehemu nzuri ya kujua,kupata haki zake, kujitambua na kuweza kujisimamia mwenyewe hususani kiuchumi ambao una kauli mbiu isemayo  'haki ya binti daima'.

Naye Dk Pastory Mondea Meneja wa Mradi wa Boresha afya (TIP)   alisema wao wamejikita katika mambo makubwa mawili usalama wa mtoto na mapambano ya Ukimwi hivyo wanashirikiana na viongozi wa dini ,vituo vya afya katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na matukio kama hayo yatakayoweza kuchochea magojwa yanayoambukizwa pia kutamua hatua zipi anapaswa kuzichukua pindi anapofanyiwa vitendo vya ukatili.

"Kuna Wananchi wengine hawajui wakitokewa na tatizo watoe taarifa wapi hivyo elimu elekezi inatolewa ili wajue watoe wapi taarifa ili sheria ichukue mkondo wake "anaeleza Mondea.

Habari Kubwa