Wazazi watakiwa kutoa ushirikiano kwa walimu kuongeza ufaulu

25Apr 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wazazi watakiwa kutoa ushirikiano kwa walimu kuongeza ufaulu

WAZAZI wametakiwa kuweka ushirikiano na walimu wa wanafunzi ili kuongeza kasi ya ufaulu wa wanafunzi nchini.

Kuwapo kwa ushirikiano huo kumeelezwa kuwa kutasaidia kufuatilia mienendo ya wanafunzi na kuwaepusha na tabia za makundi rika na hivyo kuwadanya wajikite kwenye masomo.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mwasisi wa Shule ya Huria ya Ukonga Skillful, Diodorus Tabaro, katika Mahafali ya 14  ya kidato cha sita.

Amesema ushirikiano utakaofanywa na wazazi kwa watoto wao wanaosoma kwa kiasi kikubwa utaweza kuwaongezea ufaulu.

"Shule yetu imekuwa ikimtengemea Mungu kwa mambo yote tunayoyafanya, hivyo nawahasa vijana hawa kuendelea kumtegemea Mungu wa kweli katika mitihani yao na kuamini wanafanya vizuri zaidi," amesema Tabaro.

Tabaro amesema  shule yao imekuwa ikipokea wanafunzi ambao tayari wamekata tamaa na wengine wakuwa hawamalizi shule hivyo wamekuwa msaada mkubwa kwao katika utoaji wa elimu ambapo hadi sasa tayari wametoa wanafunzi waliomaliza vyuo vikuu mbalimbali wapatao 16.

"Unajua wanafunzi tunaowapokea ni wale waliokata tamaa ambao wengi wameishia njiani kimasomo na wengine waliokata tamaa baada ya kufeli darasa la saba basi tunawachukua na kuwapa mafunzo maalum ya kujitambua kwanza alafu ndio wanaanza kusoma masomo ya darasani na hii ili kuwafanya akili zao sasa kuchangamka katika suala la masomo," amesema.

Mgeni Rasmi ambaye ni Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Jamii, Dk. Simon Mtebi, amewataka wanafunzi hao kuondoa hofu kipindi chote cha Mitihani na kuhakikisha wanamtanguliza Mungu.

Katika maafali hayo pia yalihudhuriwa na  Msimamizi Mkuu wa shule zilizopo chini ya Taasisi ya elimu ya watu wazima, Baraka Kionywaki.

Habari Kubwa