Wazazi watakiwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu

20Oct 2021
Steven William
Muheza
Nipashe
Wazazi watakiwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu

MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Halima Bulembo, amesema zaidi ya watoto 244 wenye ulemavu wilayani kwake hawajapelekwa shule.

Alitoa takwimu hizo akiwa katika Shule ya Msingi Mbaramo iliyopo Wilaya ya Muheza wakati wa hafla ya mapokezi ya mrembo wa taji la ‘Deaf Tanzania na Africa 2021’, Khadija Kanyama. Kanyama aliibuka mshindi katika shindano hiyo lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Bulembo alisema katika Wilaya ya Muheza kuna watoto takribani 341 wenye ulemavu, kata kati ya hao watoto 244 hawajapelekwa shule.

Hivyo, aliwaomba wazazi wenye watoto wao wawe chachu ya kuwapeleka shule watoto hao kwa kuwa serikali inawatambua walemavu.

Bulembo alisema kuwa serikali imepeleka Sh.milioni 80 kutoka katika fedha za corona kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa bweni la watoto wenye uhitaji maalum katika Shule ya Msingi Mbaramo.

Kwa upande wake Kanyama aliwashukuru wananchi kwa mapokezi aliyopata wakati akitokea Dar es Salaam, kwamba atakuwa bega kwa bega na serikali pamoja na wenye ulemavu.

Alisema atajitahidi kutatua changamoto zinazowakabili walemavu katika Wilaya ya Muheza huku akiwataka wazazi wasiwafiche watoto wao nyumbani ambao ni walemavu kwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za msingi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Nassibu Mmbaga alimpongeza mrembo huyo kwa kufanikiwa kupata taji hilo.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Muheza, Mashauri Kanyama, aliwaomba wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu bali wawapeleke shule.

Ofisa Elimu wa watoto wenye uhitaji maalum Wilaya ya Muheza, Sudi Wabu, alisema kwa kutambua umuhimu wa watoto wenye mahitaji maalum kupitia wananchi na wadau wa elimu wamejenga mabweni mawili mapya katika Shule ya Msingi Mbaramo.

Mbunge wa Muheza, Hamisi Mwinjuma, alisema ili kuhakikisha watoto hao wenye ulemavu wanapata elimu lazima wazazi wajenge utamaduni wa kuwapeleka shule na siyo kuwafungia ndani.

Habari Kubwa