Wazee Chadema wajitosa kikao kulinusuru taifa

14Mar 2018
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wazee Chadema wajitosa kikao kulinusuru taifa

BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), limemuomba Rais John Magufuli kuitisha mkutano wa mazungumzo kati ya serikali, viongozi wa dini, wazee na viongozi wa serikali wastaafu, ili kuzungumza mambo mbalimbali yanayoihusu nchi kwa sasa.

Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Roderick Lutembeka.

Wito wa Baraza hilo unakuja wiki chache tangu viongozi wa madhehebu mbalimbali na dini wakutane jijini na kutoa ushauri kama huo. 

Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Roderick Lutembeka wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wazee wengine wa chama hicho waliokuwapo katika mkutano huo jijini Dar es Salaam jana.

Kwa niaba ya wazee hao, Lutembeka alisema yapo mambo mengi yanayoendelea nchini hivi sasa yakiwamo ya watu kutekwa na kuuawa ambayo Chadema inaamini endapo yatafikishwa kwa Rais, yatapatiwa ufumbuzi.

"Rais Magufuli ambaye ni mzee mwenzetu, tunamuomba kwa busara za kiuongozi na hekima za uzee, akubali kuitikia wito wetu wa kukutana na wazee, viongozi wa dini na viongozi wa serikali wastaafu katika kikao cha pamoja, ili tuzungumze," alisema Lutembeka.

"Tunaamini kwamba Rais atakubali wito wetu na atakifanyia kazi kile atakachoambiwa na wazee hao wa nchi ambao atakutana nao. 

"Hata kama akiona hakuna cha kumwambia kwa sasa, lakini aamini kwamba sisi tutakuwa na kitu cha kumweleza."

Lutembeka alisema pamoja na mambo mengine ambayo wanatamani kumweleza Rais ni matukio ya kuteswa, kutekwa na kuuawa watu mbalimbali ambao wanaamini ushauri wa viongozi wa dini, wazee na viongozi hao wastaafu wa serikali na kwa hekima ya Rais ufumbuzi wake utapatikana.

Februari 21, mwaka huu viongozi wa madhehebu ya dini walikutana jijini Dar es Salaam pamoja na wanasiasa kujadili "hofu iliyotawala" miongoni mwa wananchi waliyodai inasababishwa na kutokea kwa matukio ya mauaji na watu kutekwa nchini.

Viongozi hao pia walijadili uimara wa taasisi za madhehebu ya dini, uimara wa mfumo wa serikali, pamoja na uimara wa taasisi za vyama vya siasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Katika siku za karibuni, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22)aliyefariki kwa kupigwa risasi na polisi akiwa kwenye daladala jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.

Rais John Magufuli alisema katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter Februri 11 "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."

Rais Magufuli pia alielezea kusikitishwa "sana" na kifo cha Akwilina, na kutoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo. 

Askari polisi sita wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi, ukiwamo wa kimilipuko, ili kujua bunduki iliyotoa risasi iliyomuua Akwilina, ilielezwa.

MWILI KUTUPWAAidha, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ambaye pia alikuwa katibu wa Chadema kata ya Hananasif, Daniel John, alikutwa ameuawa na mwili wake kutupwa katika ufukwe wa Coco jijini Dar es Salama Februari baada ya kutekwa mwanzoni mwa mwezi huo na watu wasiojulikana.

Akizungumza katika kikao hicho, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza alisema hofu nchini bado ipo baada ya kuwapo kwa matukio ya watu kupigwa risasi na kutekwa.

"Sijawahi kuona risasi za moto zikirushwa kwa raia, watu wanapigwa risasi mchana kweupe, sasa inatakiwa tufike mahali tuseme basi," alisema Askofu Bagonza.

Alisema viongozi wa dini wataendelea kuonya matukio kama hayo pindi yatakapotokea bila ya kujali nani yupo madarakani.

Naye Amiri Mkuu wa Baraza Kuu na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Yusuph Kundecha alisema ni kweli hofu miongoni mwa wananchi ipo baada ya kuwapo kwa matukio ambayo hawajawahi kuyaona miaka ya nyuma.

Alisema hofu hiyo inatokana na baadhi ya matamshi ya viongozi wanayoyatoa kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), James Mbatia alisema:"Tanzania bado kuna hofu, vipo viashiria ambavyo siyo vizuri.

"Kuna Watanzania wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi, akiwamo binti Akwilina. Wengine wamepotea, wengine wametekwa na kuuawa.

"Bado kuna manung'uniko, malalamiko miongoni mwa wananchi, mauaji yanatokea, Watanzania wana hofu juu ya matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu."

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kujadili lengo la 16 katika 17 ya malengo ya millennia, ambalo linahusu amani, haki na taasisi imara.

Habari Kubwa