Wazee, viongozi wa kimila wajitosa sakata la Kinana, Makamba

23Jul 2019
Godfrey Mushi
KILIMANJARO
Nipashe
Wazee, viongozi wa kimila wajitosa sakata la Kinana, Makamba

KUNDI la wazee wakiwamo baadhi ya viongozi wa mila wa mkoa wa Kilimanjaro, limejitosa katika sakata la makatibu wakuu wastaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na watu wengine mashuhuri kudaiwa kuandika waraka unaolenga kukivuruga chama hicho au kumkwamisha Rais John Magufuli.

Mwenyekiti wa wazee hao, Michael Mcha akisoma tamko lao.

Katika tamko lao lililotolewa leo na Mwenyekiti wa wazee hao, Michael Mcha, wazee hao wanadai kuwa wanaoendesha harakati hizo, wanafanya hayo wakitaka kulirejesha taifa mahali lilipotoka.

“Tunahuzunika kuona majaribio mapya ya kuturejesha tulipotoka yameanza, kazi inayofanywa na Rais kwa watanzania inaonekana ni dhahiri, hatukutegemea wae waitufikisha hapa washangilie ila sisi tunataka wautumie uzee wao kulinda amani na utulivu wa nchi, hatutakubali kugawanywa kwa tamaa binafsi za watu,”alisema Mcha

Alisema jambo pekee wanalopaswa kufanya watu hao ni kumuacha Rais aendelee kuitibu nchi na kuwapigania wasiokuwa na sauti.

Miongoni mwa wazee walioeleza masikitiko yao ni Neema Kassa, mwasisi wa CCM ambaye ameeleza kuwa hao watu wanaompiga vita ni wale waroho wa madaraka, waliozoea kula kula, kunyonya na kwa kuwa sasa wanaona Magufuli kafanya mamb mengi mazuri wanaona bora wampige vita, lakini wajue Mungu atawapiga wao vita mara 70.

“Sisi tunampongeza sana Rais Magufuli kwa kazi anayoifanya, tangu nimezaliwa sijaona kazi nzuri iliyofanywa kama anavyofanya Magufuli, maisha yangu sijawahi kusikia treni ya umeme, maisha yangu sijaona ndege nyingi zinazomilikiwa na ATCL (Shirika la Ndege Tanzania), kwa Magufuli nimeona na Mungu ambariki, ambariki.

“Labda kwa upeo wangu au labda kwa uzee wangu, niseme tu kwamba sisi wazee wa mkoa wa Kilimanjaro, tutapiga goti usiku na mchana, tutamuombea Magufuli, hao watu wanaompiga vita, watuachie Rais wa wanyonge, sisi tunampenda Magufuli kufa na kupona na tutaendelea kumuombea, misikitini tutaenda kumuomba huyu Mungu, makanisani tutaenda kumuita huyu Mungu, kumlinda Magufuli pande zote za dunia.”

Naye, Gabriel Mollel ambaye ni kiongozi wa mila (Legwanani) wa jamii ya wafugaji wa Kimasai kutoka Kata ya Kia, Wilaya ya Hai, alisema wao wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa mambo mengi anayoyafanya na wanahakikishia watanzania wao kama malegwanani, watamuunga mkono.

Kwa upande wake, Kapt. Mstaafu Haron Swai alisema tangu alipokuwa kijana wa Tanu youth League, wakati wa Uhuru, anaweza akasema Rais Magufuli ameonyesha njia katika mambo mengi ya kulipeleka taifa katika uchumi wa kati.

Kapt. Mstaafu Haron Swai.