Wazee wa baraza wataka mtuhumiwa mauaji kuachiwa

18Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wazee wa baraza wataka mtuhumiwa mauaji kuachiwa

WAZEE wa Baraza katika kesi ya mauaji inayomkabili Juma Musa, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kumwachia huru mtuhumiwa huyo kwa kuwa ushahidi wa Jamhuri haujajitosheleza kumtia hatiani.

MAHAKAMA YA KISUTU.

Wakiwasilisha hoja zao za majumuisho ya mwisho kwa nyakati tofauti, wazee hao wameiomba mahakama imwone mtuhumiwa hana hatia kwamba hakuna shahidi aliyemwona akifanya mauaji hayo.

Hoja hizo za wazee zilitolewa jana katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Naibu Msajili, Pamela Mazengo, anayesikiliza kesi ya mauaji ya kukusudia ya Fatuma Mbaga dhidi ya mume wake, Musa.

Mzee wa kwanza alidai kuwa katika ushahidi wa Jamhuri uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri, una shaka kwa sababu hakuna shahidi aliyeshuhudia mshtakiwa akifanya mauaji hayo.

Akifafanua zaidi alidai ushahidi wa Jamhuri unaeleza mshtakiwa alionekana siku ya tukio akiwa amebeba begi na kutoweka nyumbani kwake.

Hata hivyo, katika utetezi wake alidai kuwa alisafiri kwenda mkoani Mwanza kumuuguza baba yake mzazi, na baadaye alifariki.

Mshtakiwa alidai kabla ya kusafiri kwenda Mwanza, alimwacha mke wake akiwa mzima na kwamba siku ya pili yake Mei 12, 2015 alipigiwa simu na mwenyekiti wa serikali ya mtaa akimjulisha kwamba mke wake amefariki kwa kupigwa shoti ya umeme.

Pamoja na mambo mengine, uchunguzi wa Jamhuri ulibaini kwamba baba mzazi wa mshtakiwa yupo hai na ni mwajiriwa wa Kiwanda cha Nguo Mwanza (Mwatex).

Alidai mashahidi wote wa Jamhuri waliiambia mahakama kwamba waliukuta mwili wa Fatuma ukiwa kitandani na pasi ya umeme ikiwa pembeni yake.

Mzee wa pili, alidai kuwa ushahidi wa Jamhuri una shaka kwa sababu hakuna shahidi aliyemshuhudia mshtakiwa akimuua Fatuma.

Pia alidai kuwa ushahidi wa mshtakiwa umedai kuwa alipata taarifa kwamba mke wake alikufa kutokana na shoti ya umeme, lakini mwili ulikutwa na majeraha sehemu za siri na uti mgongo umevunjika, mambo ambayo hayahusiani na umeme.

Alidai Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kama kweli baba mzazi wa mshtakiwa ni mwajiriwa wa Mwatex na pia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walikwenda eneo la tukio kuthibitisha kama kulikuwa na shoti ya umeme siku ya tukio au la.

Mzee wa tatu, alidai ushahidi wa Jamhuri umeshindwa kuieleza mahakama kwamba nani alifanya mauaji hayo na kama ni mtuhumiwa nani alimwona.

Wazee hao kwa nyakati tofauti waliiomba mahakama imwachie huru mshtakiwa kwa sababu hakuna ushahidi wa kuthibitisha kosa hilo dhidi yake.

Msajili Mazengo alisema baada ya kusikiliza hoja za majumuisho ya wazee wa baraza na pande zote mbili, mahakama yake itapanga tarehe ya kusoma hukumu na itawajulisha.

Katika kesi ya msingi, Musa anadaiwa kuwa Mei 11, 2015 eneo la Mchikichini, jijini Dar es Salaam, alimuua kwa makusudi mke wake Fatuma Mbaga.

Habari Kubwa