Wazee wa kanisa watakiwa kushirikiana na viongozi wa dini

10Aug 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Wazee wa kanisa watakiwa kushirikiana na viongozi wa dini

Wazee wa Kanisa la Moravian Tanzania kutoka usharika mbalimbali mkoani Mwanza wametakiwa kushirikiana na Wachungaji na Wainjilisti ili kuweza kutangaza injili na kudumisha amani kwa watu na taifa kwa ujumla.

Askofu Ezekiel Yona.

Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa hilo Jimbo la Magharibi, Askofu Ezekiel Yona wakati wa hafla ya kuzindua Studio katika Usharika wa Nyakato wilayani Ilemela mkoani Mwanza ulioenda sambamba na tukio la kusimika wazee wa kanisa hilo kutoka ushirika wa Nyakato, Igoma, Igombe uliofanyika katika. 

Askofu Yona, amesema ili kuendeleza kazi ya Mungu, kulinda amani na kuleta maendeleo ya taifa wazee hao wahakikishe wanashirikiana na wachungaji na wainjilisti pamoja na kuwa washauri wazuri kwa viongozi wao na siyo kuwasemea pembeni pale wanapo kosea.

"Naupongeza Ushirika wa Nyakato kwa kuweza kufungua studio kwani wamefanya kazi nzuri ya kupeleka injili ya Bwana kwa watu kupitia rasilimali hiyo"alieleza Askofu Yona.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Moravian Ushirika wa Nyakato, Mchungaji Stephen Mhenga amesema mradi huo wa ujenzi wa studio umegharimu zaidi ya milioni 55 mpaka ulipofikia,ulikua unahitajika fedha nyingi  na walianza kujipanga kwa sababu waliona ikikamilika itasaidia kuondoa utegemezi wa wanakwaya kwa kanisa kupitia waumini.

"Kusudi letu katika studio hii ni mambo mawili la kwanza ni kutangaza injili kwa njia ya uimbaji kwani tunategemea kwaya nyingi zitatoka maeneo mbalimbali kutoka mikoa yote ya nchini Tanzania,mpaka sasa tuna oda ya kwaya sita kutoka mikoa ya Tabora,Shinyanga,Musoma,jambo hili ndio lililotusukuma kufanya kasi ya kutafuta fedha za kukamilika studio hii,"amesema Mchungaji Mhenga na kuongeza kuwa;

"Jambo hilo limekuwa kusudi jema kwa watakao rekodi kupitia studio hiyo nyimbo zao watakazoimba watakuwa wametusaudia kutangaza injili huku kusudi la pili ikiwa ni uchumi tumeona sana kwaya yetu inategemea kanisa,hivyo tukaona wakiwa na mradi huu utawasaidia kukusanya fedha ambazo zitawasaidia katika mambo mengine na kuboresha uimbaji wao,"amesema.

Naye Mwenyekiti wa kwaya ya Nyakato Moravian Ambilike Kyamba, amesema kwaya hiyo imefanya uzinduzi wa studio yake ambao wanategemea mambo mengi pamoja na kuwa chanzo cha kuinua uchumi wa kwaya hiyo na kanisa kwa ujumla kwani wameona vijana wengi wakipotea kutokana na hali duni ya uchumi.

Kyamba amesema,kupiti studio hiyo vijana wataajiriwa hivyo kuwa wamewaepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu,kuwa tegemezi na kuinua pato la taifa.

Mwalimu wa kwaya hiyo,Obedi Malando, amesema studio hiyo imetengenezwa kwa ajili ya kuwaleta karibu watu na kwa manufaa ya wengi katika kueneza injili,pia itarekodi vikundi vyote na watu wote wanaoimba nyimbo za injili tu,pia ni fursa kwa  wakazi wa Kanda ya Ziwa  kukuza na kuibua vipaji mbalimbali vya kwaya na binafsi.

Hata hivyo mmoja wa wanakwaya wa kwaya hiyo Rehema Ernest, amesema wanamshukuru Mungu kwa kuweza kuzindua studio yao kwani awali walikuwa na changamoto ya kujumuika na watu wengine ambao wanaimba nyimbo ambazo siyo za injili pia kushindwa kupata fedha kwa ajili ya kurekodia kazi zao.

Habari Kubwa