Wazee waikubali 'Hapa Kazi Tu'

14Feb 2016
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Wazee waikubali 'Hapa Kazi Tu'

WAZEE wa Mkoa wa Dar es Salaam, wamempongeza Rais John Magufuli na kumweleza kuwa wameridhika na kasi aliyoanza nayo ndani ya siku 100 za kwanza za utawala wake, na kwamba hiyo imedhihirisha kuwa Watanzania walifanya uamuzi sahihi kumchagua.

Walitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano baina yao na Rais Magufuli katika ukumbi wa Diamond Jubelee.

Akisoma tamko hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Hemedi Mkali, alisema wazee wengi wamefurahishwa na kasi yake na wamemwomba asitetereke kwani wote wako nyuma yake.
Rais Magufuli aliingia kwenye kampeni za uchaguzi na msemo wa 'Hapa Kazi Tu'.

“Tulikuwa tunafuatilia utendaji wako, umedhihirisha kwamba Watanzania walifanya uamuzi sahihi na wa busara wewe uwe Rais wao,” alisema Mkali.

Aidha, wazee hao walimweleza kuwa wataendelea kuwa bega kwa bega nae katika kurejesha nidhamu pamoja na utamaduni wa uwajibikaji serikalini.

“Umakini wa utendaji wako umejidhihirisha kwenye uteuzi wa watendaji wako, Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu, mpaka sasa umewadhihirishia Watanzania na ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi iliyokomaa kisiasa,” alisema.

Aidha, walimweleza kuwa katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kufungua Bunge la 11 ilitoa mwongozo ya Tanzania wanayoitarajia.

Pia walimsifu kwa kasi yake aliyoonyesha katika kutumbua majipu kwenye maeneo tofauti ya kazi pamoja na kutekeleza ahadi yake ya elimu bure na kuboresha sekta ya afya ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

“Uliahidi kubana matumizi na kwenye safari za nje tu umeokoa Shilingi bilioni 7, juzi uliahidi kutoa Shilingi bilioni 12 kusaidia kesi mahakamani umetekeleza ndani ya siku nne," alisema. "Tunakupongeza sana wewe ni jemedari kweli kweli."

Aidha, walimpongeza kwa kutimiza ahadi yake ya kuwabana wakwepaji kodi, kuongeza ukusanyaji wa mapato serikali huku wakimweleza kuwa haijapata kutokea kwani hatua hizo zimerudisha matumaini ya watanzania.

“Tuliomba tukutane nawe ili kukueleza kuridhishwa kwetu na kasi yako, hatukutaka kukupa changamoto zetu ingawa zipo ndogo ndogo, tunaomba tujenge utamaduni wa kukutana mara kwa mara ili tukushauri na kukuelezea hali halisi, ili kukusaidia katika kujenga Tanzania mpya,” alisema Mkali.

Habari Kubwa