Waziri Kairuki: Serikali imeandaa mazingira ya uwekezaji

01Jul 2020
Allan lsack
ARUMERU
Nipashe
Waziri Kairuki: Serikali imeandaa mazingira ya uwekezaji

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Uwekezaji, Angellah Kairuki, amesema kwa kipindi cha miaka mitano serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji nchini, ili kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kilimo cha mbegu na maua ya Fides Tanzania, Bas Van Lankveld, wa kwanza kulia, akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki, wa katika kuhusu maendeleo ya maua kwenye shamba, na wa mwisho kushoto ni Mkurugenzi wa Tanzania Horticultural Association (Taha), Jacquelin Mkindi. Picha : Allan lsack

 

Kairuki aliyasema hayo, juzi wakati wa ziara yake ya kikazi Wilaya ya Arumeru, alipotembelea mashamba ya makampuni saba ya kilimo cha mboga, matunda, maua, viungo na mbegu.

Alisema ili kuvutia na kuongeza uwekezaji nchini, serikali imeondoa baadhi ya sheria zilizokuwa kikwazo kwa wawekezaji pamoja na kufuta baadhi kodi mbalimbali.

Alisema kwa sasa uchumi wa nchi, unaendelea kukuwa kwa kasi kutokana ongezeko la wawekezaji wa kubwa na wa kati kuwekeza kwenye sekta mbalimbali husasni ya kilimo.

Kairuki, ameitaka sekta ya kilimo cha mboga,matunda na maua washirikiane na mabalozi wa Tanzania, kutafuta masoko ya mazao hayo nje ya nchi.

“Rais Magufuli alivyoingia madarakani alikuta sekta hii, mauzo yake yalikuwa dola  kimarekani milioni 412 kwa mwaka, lakini sasa hivi mauzo yamepanda hadi kufikia dola ya kimarekani milioni 779,”alisema Kairuki.

Licha ya kuzungumza hayo, alisema sekta hiyo, itaongeza mapato ya nchi, endapo makampuni ya kilimo cha mboga, maua na matunda yataongeza uwekezaji na kuzingatia ubora wa bidhaa kulingana na mahitaji ya soko na walaji.

Alisema serikali ipo tayari kuwasilikiliza wawekezaji kuhusu na matatizo mbalimbali yanayowakabili ili kutafuta njia mbadala ya kutatua matatizo hayo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Murro, alitumia fursa hiyo, kumshukuru Rais Magufuli kwa kufuta tozo zaidi ya 150, ambazo zilikuwa kikwazo cha kuchelewesha maendeleo katika sekta ya uwekezaji.

Muro, aliahidi kuendelea kuweka na kuandaa mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji wilayani humo, kwa kuwa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo unategemea kilimo.

Aliongeza kuwa kati ya mashamba saba ya kilimo cha maua na matunda yaliyokufa wilayani humo, serikali imeshayarudisha mashamba matatu na watashirikiana na wawekezaji kuwekeza kwenye mashamba hayo.

“Tumeshampata mwekezaji mwenye mtaji wa fedha kiasi cha dola za kimarekani bilioni tatu muda siyo mrefu tutaanza uwekezaji kwenye mashamba hayo,alisema Muro.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Horticultural Association (TAHA), Dk. Jaquelin Mkindi, alisema wamefanikiwa kuibadilisha sekta ya mboga,matunda,maua na viungo awali kutoka kiasi cha dola za kimarekani milioni 60, hadi kufikia dolla za kimarekani milioni 780 kwa mwaka.

Alisema serikali kwa kushirikiana na Taha na makampuni mengine ya kilimo, kwa pamoja walishirikiana kuondoa zaidi ya sheria 50, zilizokuwa kikwazo katika sekta ya kilimo.

Aidha alisema wa kipindi cha miaka mitano,uchumi wa Tanzania umekuwa kwa kasi kati ya nchi 10, duniani kwa mujibu wa taarifa ya Banki ya Dunia ya mwaka 2019.

“Sekta hii tumefanikiwa kukua kiuchumi kutoka dolla za kimarekani 400,000 hadi kufikia dolla za kimarekani 779,000 kwa mwaka na matarajio yetu miaka mitano ijayo sekta hii itakuwa kiuchumi hadi kufikia dolla za kimarekani billion tatu,”alisema  Jaquelin.

Mbali na kuzungumza hayo, Jaquelin, alisema kati ya Wilaya nchini, zenye mashamba makubwa ya kilimo cha mboga, matunda na maua ni Wilaya ya Arumeru, lakini ndani ya Wilaya hiyo, kwa kipindi cha miaka 10, mashamba mengi yamekufa na kupoteza ajira nyingi kwa wafanyakazi, hivyo ameiomba serikali kufufua mashamba hayo.

Habari Kubwa