Waziri aagiza kukamatwa bosi wa pori

12Jul 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri aagiza kukamatwa bosi wa pori

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Katavi kumkamata na kumfungulia mashtaka Mkuu wa Kanda - Pori la Akiba Rukwa, Emannuel Barabara kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla AKITOA MAAGIZO.

Waziri Kigwangalla amefanya uamuzi huo ikiwa ni miezi mitatu tangu alipomsimamisha kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo, ambazo alisema zimethibitishwa kupitia taarifa za kiuchunguzi.

Waziri Kigwangalla alitoa agizo hilo jana baada ya kupokea taarifa ya Wilaya ya Mlele iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Wilaya hiyo, Rachel Kasanda, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Alisema Barabara anatuhumiwa kwa vitendo vya uhujumu uchumi kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo, na kushirikiana na majangili kuruhusu uvunaji holela wa rasilimali za misitu ndani ya pori hilo kwa maslahi yao binafsi.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda, alisema katika kipindi cha Desemba 2017 hadi Februari 2018, kamati yake ya ulinzi na usalama ilipata taarifa za uvamizi mkubwa katika Pori la Akiba Rukwa ambapo iliamua kufanya operesheni maalum iliyosaidia kukamata watu 22 waliokuwa wakichana mbao na kukamata mbao 5,122, slipa 924 na magogo 188.

 

Alisema kwa kiasi kikubwa uhalifu huo ulichangiwa na Barabara ambaye hakutaka kuweka wazi uhalifu uliokuwa ukifanyika ndani ya pori hilo kwa kamati yake ya ulinzi na usalama, badala yake aliiaminisha kuwa mambo ni shwari.

 

Kadhalika, Dk. Kigwangalla aliagiza maofisa na askari wote 34 wa Pori la Akiba Rukwa kurudishwa makao makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ili kupangiwa kazi nyingine, ambapo kabla ya zoezi hilo ameagiza wahojiwe na Takukuru kuhusu mwenendo wa vitendo vya Barabara na endapo nao watathibitika kuhusika wafunguliwe mashtaka ya kushirikiana nae katika tuhuma zinazomkabili.

 

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla amemsimamisha kazi, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu wa Wilaya ya Mlele, Ezeckiel Mbilinyi na  watumishi wengine watatu kwa kile alichokieleza kuwa ni uzembe wa kushindwa kusimamia vizuri rasilimali za misitu wilayani humo, sambamba na tuhuma za kushirikiana na Barabara kuhujumu rasilimali za misitu kwa kutoa vibali na kugonga nyundo (mihuri) rasilimali hizo zilizokuwa zikivunwa kinyume cha sheria kwenye maeneo ya hifadhi.

 

Aidha, Dk. Kigwangalla alitangaza kusimamisha utoaji wa vibali vipya vya uvunaji na usafirishaji wa mbao na magogo kwa mikoa ya kanda ya magharibi ikiwamo Katavi na Tabora kwa miezi mitatu mpaka hapo utaratibu mzuri utakapowekwa wa kudhibiti uvunaji wa rasilimali hiyo kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria.

 

 

Habari Kubwa