Waziri aagiza mamlaka ya bandari kukamilisha miradi mapema

15Jan 2022
Adela Madyane
Kigoma
Nipashe
Waziri aagiza mamlaka ya bandari kukamilisha miradi mapema

Waziri wa ujenzi na uchukuzi Prof Makame Mbarawa ameagiza mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) kushirikisha wataalamu ili kuhakikisha miradi ya ujenzi wa bandari inakamlika kimamilifu na kwa ubora unaostahili.

Waziri Mbarawa akifafanua jambo wakati wa kutembelea mradi wa ujenzi wa chelezo

Amesema kumekuwa na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya bandari licha ya pesa za ujenzi kutolewa jambo ambalo linachelewesha maendeleo kwa wananchi.

Akitoa agizo hilo alipotembelea ujenzi wa bandari ya Kibirizi na Ujiji zilizopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma  ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi na usimamizi wa miradi chini ya TPA  yenye thamani ya shilingi billion 32.

"Mamlaka ya Bandari lazima iwe na miongozo ya usimamizi wa miradi ili iiishe kwa wakati, haiwezekani bandari hii ichukue miaka 3 toka 2019 mpaka sasa bado haijakamiki, hii haikubaliki, lazima kuwe na mikutano ya mara kwa mara na wakandarasi na muhandisi mshauri ili kuepuka shida ya kuchelewesha miradi, lakini pia tusiipange kwa kuangalia leo tu, tuangalie miaka 100 ijayo ili kuwe na miradi endelevu na yenye thamani" Ameeleza Mbarawa.

Zaidi ameelekeza ujenzi wa chelezo kuwa chini ya Shirika la Meli (MSCL) kwakuwa kazi  kuu ya Marine ni kutengeneza meli huku kazi kuu ya bandari ikiwa ni kupakia na kupakua mizigo hivyo kila mamlaka ifanye shughuli yake husika.

Prof Mbarawa amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bandari ya Kibirizi na Ujiji  ulioanza March 2019 ambapo mpaka sasa bandari ya Kibirizi ina asilimia 63 na bandari ya Ujiji kwa asilimia 34 , ulitakiwa kuisha mwezi November 2021.

Kwa upande wa Kaimu meneja wa TPA mkoani Kigoma  Manga Gassaya amekiri kuchelewa kwa miradi hiyo na kusema kuwa watahakikisha kuanza utekelezaji wa miradi hiyo haraka iwezekanavyo kwa kukaa na wakandarasi kwaajili ya ufanisi wa miradi hiyo.

Naye Ramadhan Mwamandiga amesema kuwa changamoto iliyosababisha kushindwa kutekeleza miradi hiyo kwa wakati ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha ongezeko la maji la takribani 1.5  katika eneo la utekelezaji wa mradi pamoja na Mkandarasi kushindwa kukamilisha usanifu kwa baadhi ya maeneo ya mradi.

Kwa upande wake Issa Mustafa mwenyekiti wa Mabaharia mkoani Kigoma amesema endapo bandari itaisha itasaidia usalama wa vyombo vyao kwani bandari wataweza kuwalipa pale uharibifu unapotokea.

"Tunataka tufanye kazi kwa weledi, kila mkandarasi akija anasema tuhamie huku, mara magati hayapo, tunaomba serikali itusaidie kupata bandari itakayotusaidia kuwa salama sisi na vyombo vyetu bandari hii iishe kwa wakati" Amesema Mustafa.

Amesema furaha ya wanakigoma ni kupata bandari, mvua zikinyesha maji yanatuama kwenye bandari , gari zinazoleta mizigo ni changamoto, sisi tunaosubiri mizigo kwenye maboti yetu ni changamoto pia, na hata kwa makuli wanaosubiri mizigo na kusisitiza kuwa endapo bandari itakamilika itawasaidia kufanya kazi kwa weledi na kujiingizia kipato zaidi.