Waziri aagiza upimaji shamba hekta 2,000

19Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Ukerewe
Nipashe
Waziri aagiza upimaji shamba hekta 2,000

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupima na kupatiwa hati shamba lake la miti la Rubya, wilayani Ukerewe lenye ukubwa wa hekta 1,926.3.

Dk. Mabula alitoa agizo hilo juzi wakati alipokwenda kukagua ujenzi wa nyumba za watumishi wa TFS unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika ziara ya siku moja katika kisiwa cha Ukerewe kufuatilia utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika hamashauri za mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Alisema kinachohitajika sasa kwa TFS ni kuhakikisha shamba hilo linapimwa na kupatiwa hati itakayoonyesha mipaka halisi ili kuepuka migogoro.

''Miji inakua na wananchi bado wanahitaji maeneo. Bila kuwa na hati inayoonyesha mipaka ya shamba kunaweza kuleta migogoro. Tuelewe hati inalinda mipaka ya shamba lisivamiwe na wananchi,” alisema.

Naibu Waziri pia aliagiza eneo la shamba kuwa mpango kina utakaoonesha kila matumizi ya sehemu ya ardhi kwa kuwa katika eneo hilo mbali na shamba la misitu kuna makazi ya watu.

Meneja wa Shamba hilo, Festo Chaula, alimweleza Naibu Waziri Rubya ni miongoni mwa mashamba 23 yanayomilikwa na TFS lililoanzishwa mwaka 1951 kwa Tangazo la Serikali Namba 230.

Alisema wakala pia ina eneo lingine lilipandwa miti kwa ubia na halmashauri ya wilaya ya Ukerewe lenye ukubwa wa hekta 1,152 lenye miti aina ya misindano.

Kwa mujibu wa Chaula, katika kuboresha makazi ya watumishi wa wakala, Sh. milioni 383.8 zimetengwa katika mwaka wa fedha wa 2019/20 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba tatu, tangi la kuhifadhia maji, ukarabati wa nyumba mbili na ujenzi wa uzio wa bustani ya miti, kazi ambayo ilianza Agosti, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Dk. Mabula ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Ukerewe kupima maeneo katika halmashauri hiyo kama operesheni maalum ili kuondoa migogoro ya ardhi sambamba na kuondoa ujenzi holela.

Akizungumza na madiwani pamoja na watumishi wa ardhi katika halmashauri hiyo, Dk. Mabula alisema halmashauri hiyo ina vifaa vya upimaji, hivyo kinachotakiwa kwa sasa ni kuwasiliana na ofisi ya Ardhi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupatiwa wapimaji.

Habari Kubwa