Waziri afuma simu, mihadarati gerezani

23Mar 2019
Nebart Msokwa
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri afuma simu, mihadarati gerezani

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amebaini kuingizwa kwa simu na dawa za kulevya ndani ya Gereza la Ruanda mkoani Mbeya kwa ushirikiano kati ya askari na wafungwa.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, picha mtandao

Kutokana na hali hiyo, amemwagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike, kuwasimamisha kazi askari wanne wa Gereza la Ruanda jijini Mbeya kwa tuhuma za kushirikiana na wafungwa kuingiza simu na dawa za kulevya.

Masauni alitoa agizo hilo jana, alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, huku akisema alibaini ukiukwaji mkubwa wa sheria na maadili ya magereza kwenye gereza hilo.

Alisema alibaini wafungwa wanamiliki simu tisa na dawa za kulevya aina ya bangi ndani ya gereza na kwamba vyote vilikuwa vimeingizwa kwa ushirikiano kati ya askari wasiokuwa waaminifu na wafungwa.

Aliwataja askari hao wanaotakiwa kusimamishwa kazi kuwa ni Inspekta Longino Mwemezi, Ramadhan Mhagama, Alexander Mwinjano na Benjamini Malango ambao wote ni masajini taji wa Magereza.

Alisema baada ya kuzinasa simu hizo alizikabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi na kwamba taarifa za awali zilionyesha kuwa simu hizo zilikuwa zinatumika kwenye vitendo vya uhalifu ikiwamo rushwa.

“Namwagiza pia Kamishna Generali wa Magereza kuunda tume ya kuchunguza vitendo hivyo, ili kubaini mtandao mzima uliokuwa unahusika na wakibainika wengine hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Masauni.

Alisema vitendo vya aina hiyo vilishakemewa na Rais John Magufuli na aliagiza vidhibitiwe ndani ya magereza yote nchini ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

Alisisitiza kuwa vitendo hivyo ni hatari kwa usalama wa magereza endapo askari wataendelea kutokuwa waaminifu kwa kuruhusu viendelee kufanyika ndani ya magereza.

Naibu Waziri Masauni aliwataka wakuu wa magereza yote nchini kuwa makini kwa kuzuia vitendo hivyo vya ukiukwaji wa sheria na maadili ili kulinda usalama wa maeneo hayo ambayo ni hatarishi. Masauni alifanya ziara ya siku mbili mkoani Mbeya.

Mbali na kutembelea gereza la Ruanda na kuzungumza na wafungwa, pia alitembelea Gereza la Kilimo la Songwe kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la wafungwa kutumika kwenye uzalishaji.

Habari Kubwa