Waziri afunguka mauaji ya Watanzania Msumbiji

10Jul 2019
Romana Mallya
Nipashe
Waziri afunguka mauaji ya Watanzania Msumbiji

KUTOKANA na mauaji ya Watanzania tisa nchini Msumbiji, serikali imewataka wananchi kufuata sheria za nchi kwa kuzingatia taratibu zilizopo za kuvuka mpaka kwenda nchi nyingine ili iwe rahisi kusimamia usalama wanapopatwa na matatizo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.

Mauaji hayo yalitokea mwishoni mwa mwezi uliopita katika kijiji cha Nkole kilichopo upande wa Msumbiji ambapo pia raia wengine wawili wa nchi hiyo nao walipoteza maisha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kihamba mkoani Mtwara, kuhusiana na tukio hilo ambalo Watanzania hao walikuwa Msumbiji kwa shughuli za kilimo cha mpunga.

“Nawaomba mfuate sheria za nchi yetu kwa kutumia utaratibu uliowekwa wa kuvuka mpaka mmoja kwenda nchi nyingine ili iwe rahisi kusimamia usalama wenu,” alisema na kuongeza:

“Serikali inaendelea kuhakikisha hatulali usingizi hadi wahalifu wote wakamatwe. Ili muendelee kufaidi matunda ya serikali hii nawaomba mtoe ushirikiano wenu kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu watu mnaowatilia mashaka ili zifanywe kazi.”
Hata hivyo, alisema waliofanya mauaji hayo mpaka sasa hawajapatikana, na kusisitiza kuwa watakamatwa.

“Nimeona nizungumze hayo mambo mawili muhimu kwenu, mengine tuachieni Serikali tutahakikisha tunaviwezesha vyombo vyetu hususani katika maeneo haya, nyinyi ni mashahidi kuwa hali ya usalama katika nchi hii ni nzuri,” alisema.

Masauni alisema serikali itahakikisha kila inavyoweza kufanywa inalinda usalama na maisha ya wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla.

“Serikali haiko tayari kuona uhai wa raia wake ukichezewa tunawahakikishia wananchi ulinzi na usalama lakini na nyie mtoe taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pindi mnapotilia shaka mtu yoyote ili uhalifu udhibitiwe,” alisema.

Mauaji hayo yalitokea mwishoni mwa mwezi uliopita wakati Watanzania hao wakiwa shambani wakilima mpunga walivamiwa na watu wasiofahamika wenye silaha, na kuwashambulia na kusababisha vifo hivyo na kujeruhi Watanzania wengine sita.

Habari Kubwa