Waziri ageuka mbogo kuwajibika

25Sep 2018
Na Mwandishi Wetu
UKARA
Nipashe
Waziri ageuka mbogo kuwajibika

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, jana aligeuka `mbogo’ baada ya kuulizwa iwapo yuko tayari kuwajibika kwenye nafasi hiyo baada ya kutokea uzembe uliosababisha tukio la kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe.

Akiwa katika kijiji cha Ukara wilayani Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, waandishi wa habari walimuuliza waziri huyo kuhusu maoni ya wadau mbalimbali wanaohoji waziri huyo kuendelea kuwapo kwenye nafasi hiyo, wakati kuna uzembe umefanyika uliosababisha zaidi ya watu 200 kupoteza maisha.

Swali hilo lilionekana kumkera Waziri Kamwelwe na kugeuka `mbogo’ huku akiwakemea waandishi waliomzunguka kwa kuwaambia anawashangaa kwa kukosa moyo wa huruma.

“Tupo katika masuala ya uokoaji na msiba nyie mnaleta masuala ya kisiasa, hilo siyo swali, nashangaa watu wapo katika majonzi nyie hamuonyeshi majonzi,” alijibu Kamwele ambaye alionekana kuwa na hasira.

Hata hivyo, mmoja wa waandishi waliokuwapo eneo hilo alipoendelea kumuuliza maswali waziri huyo, alijibiwa kuwa “mkiendelea kuuliza nitawaweka lockup (mahabusu).”

Tangu kuzama kwa kivuko hicho Alhamisi iliyopita, serikali imekuwa ikichukua hatua za kuwawajibisha baadhi ya watendaji waliokuwa wakikisimamia kivuko hicho.

Juzi, Rais John Magufuli alitangaza kuivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Brigedia Jenerali mstaafu, Mhandisi Mabula Mashauri.

Kadhalika jana Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mhandisi Dk. John Ndunguru, pamoja na kuivunja bodi hiyo.

Pia, jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa kijiji cha Ukara alitangaza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Temesa, Mussa Mgwatu, ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo la kuzama kwa kivuko.

Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kutochukuliwa hatua kwa waziri anayehusika na sekta hiyo ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia vivuko vyote nchini.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika kuwa “Nchi zenye ustaarabu! Kwetu kutaka uwajibikaji inakuwa nongwa. Ferry inapata ajali saa nane, saa matatu zinapita bila Kamati ya Ulinzi na Usalama kukaa. Mkuu wa mkoa yupo. Waziri wa Mambo ya Ndani yupo. Waziri wa Uchukuzi yupo.”

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alihojiwa na vyombo vya habari alimwomba Rais Magufuli kuwachukulia hatua watu wote waliohusika na kutokea kwa ajali hiyo.

Mbowe aliomba Rais Magufuli kuchukua hatua dhidi ya Polisi, Sumatra, Temesa na Navy na wengine kwa kuhoji walikuwa wapi na hata uokoaji kuchelewa hadi wavuvi wadogo wasiokuwa na vifaa waanze kuokoa.

Habari Kubwa