Waziri agoma msamaha kodi kwa gari la kifahari

21May 2022
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Waziri agoma msamaha kodi kwa gari la kifahari

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Fedha na Mipango, Saada Mkuya Salum,  amesema wizara imekataa kutoa msamaha wa kodi ya Sh. milioni 308.5 kwa gari la kifahari aina ya Benzi.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Fedha na Mipango, Saada Mkuya Salum.

Gari hilo ni la Kampuni ya Turkys Mifuko inayomilikiwa na mfanyabiashara Toufky Salum Turky na kwamba maombi ya msamaha huo yalikuwa kinyume cha Sheria ya Uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa babari ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar, Waziri Saada  alisema msamaha wa kodi kwa wawekezaji unapaswa kutolewa wakati wa ujenzi wa mradi na siyo baada ya mradi kukamilika na kuanza kuzalisha.

“Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu, maombi yake ya msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Mifuko Turky yalikataliwa na waziri kwa sababu yameletwa kinyume na sharia, mradi ukiwa tayari umeanza uzalishaji kinyume na sheria.,”alisema Waziri Saada.

Alisema kwa mujibu wa sharia, mwekezaji anaweza kunufaika na msamaha wa kodi wakati wa ujenzi wa mradi, lakini baada ya mradi kukamilika na kuanza uzalishaji, fursa ya msamaha wa kodi inakuwa imemalizika.

Alisema kwa msingi huo, ndiyo maana Wizara iliamua kuyatupa maombi ya kampuni hiyo ya kutaka msamaha wa kodi.

“Wizara kazi yetu kubwa kusimamia sheria, taratibu na mifumo hatuwezi kufanya mambo kinyume cha sheria hasa katika suala la kusimamia mapato ya serikali,“ alisisitiza.

Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar, Juma Hasssan Hassan, alisema baada ya maombi yao wanatakiwa kurudi TRA kulipa kiwango hicho cha kodi.

Alisema TRA inaendelea kuwafuatilia kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kusimamia sheria ili kuhakikisha fedha hizo zinalipwa baada wa waziri kukataa kutoa msamaha wa kodi wa gari hilo la kifahari.

Kaimu Meneja Uhusiano na Elimu kwa Walipakodi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Makame Khamis Mohamed, alisema gari hilo limesajiliwa na kupewa namba Z-1 kutokana na wahusika kulipa Sh. milioni 15 baada ya kuingizwa Januari, mwaka huu.

Alisema kama gari linatembea mitaani, watakuwa wanavunja sheria kwa sababu hairuhusiwi kutembea kabla ya kukamilisha malipo ya kodi.

Habari Kubwa