Waziri ahamasisha ufugaji nyuki

22Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Ukerewe
Nipashe
Waziri ahamasisha ufugaji nyuki

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, amehamasisha wakazi wa kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza kufuga nyuki kutokana na faida ya asali kiuchumi na kiafya.

Pia Kanyasu ametoa ruhusa kwa wananchi wenye nia ya kufuga nyuki kuitumia misitu ya hifadhi mitano iliyoko katika kisiwa hicho inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Kanyasu alitoa ruhusa hiyo kutokana idadi kubwa ya watu katika kisiwa hicho huku kukiwa na ufinyu wa ardhi.

Alisema lengo la kutoa hamasa na ruhusa hiyo ni kuwasaidia wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kuanza kufuga nyuki kibiashara badala ya kulima na kuvua samaki pekee.

Akizungumza juzi na kikundi cha watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na useremala wa kutengeneza mizinga ya nyuki ya kisasa mjini Nansio, Naibu Waziri alisema misitu hiyo mitano yenye hekta 1,300 itawasaidia kuitumia kufuga nyuki kibiashara.

Naibu Waziri alisema kutokana na ongezeko kubwa la watu katika kisiwa hicho chenye mita za mraba 700 ambao sasa wanakadiriwa kufikia 400,000 wakazi hao wana kila sababu ya kujiingiza kufuga nyuki.

Aliwaambia wananchi hao kuwa kutokana na ardhi ya kilimo kuchoka pamoja na kupungua kwa samaki kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu, njia mbadala ni kufuga nyuki kutokana na mahitaji makubwa ya asali ndani na nje ya nchi.

Kanyasu aliwahakikishia uwapo wa soko la uhakika kutokana na mahitaji makubwa ya asali China na Marekani. Alisema Tanzania bado haijakidhi mahitaji ya soko hilo.

Kwa mujibu wa Kanyasu, China pekee inahitaji tani 600,000 za asali lakini kutokana na uzalishaji duni, Tanzania bado haijasafirisha hata nusu tani ya asali inayohitajika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Esther Chaula, ameahidi kutoa mkopo kwa kikundi hicho cha watu wenye ulemavu ili watengeneze mizinga mingi itakayowezesha upatikanaji wa kutosha kwa ajili ya kufugia nyuki.

Alisema ufugaji wa nyuki katika misitu hiyo ya TFS utatoa ahueni ya ulinzi shirikishi kwa vile wananchi wataona faida ya moja kwa moja kupitia asali wanayoipata.

Katika hatua nyingine, Kanyasu aliiagiza TFS kuhakikisha inanunua mavazi maalum ya kurinia asali na kuyasambaza katika vituo ambayo wananchi watakuwa wakiyaazima wakati wa kurina asali badala ya kuendelea kutumia moto wakati wa kurina.

Alisema takribani nyuki bilioni moja kila mwaka huuawa kwa moto kutokana na urinaji huo ambao si rafiki wa mazingira.

Habari Kubwa