Waziri aibana NHIF malipo hospitali

23Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri aibana NHIF malipo hospitali

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kulipa madeni ya hospitali zinazotoa huduma za bima ndani ya mwezi mmoja.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, picha mtandao

Ummy alitoa agizo hilo jana, jijini Dar es Salaam, baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi, kusema hiyo ni changamoto wanayokutana nayo katika utoaji wa huduma kwenye jengo la huduma binafsi lililozinduliwa hospitalini hapo.

Mtendaji mkuu huyo alieleza changamoto hiyo wakati wa uzinduzi wa jengo la kutoa huduma binafsi za kibingwa kwa wagonjwa wa nje.

Msangi alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo kwenye utoaji wa huduma binafsi ni ongezeko la wagonjwa, hivyo mifuko ya bima ya afya, ukiwamo NHIF usipotoa malipo kwa wakati husababisha shida kwao.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Ummy, wakati akizindua jengo hilo, alisema alishaielekeza NHIF kwamba kama mtu ameshatoa huduma kwa wateja, alipwe ndani ya mwezi mmoja.

“NHIF mpo hapa? Nataka ndani ya mwezi mmoja muwe mmewalipa watoa huduma kwa wanachama wenu. Kama mtu amefanya kazi mjitahidi mumlipe, maana mnajificha kwenye kivuli cha kuhakiki. Mnahakiki kitu gani kisichoisha?” Alihoji.

“Nanawaomba na nyie watoa huduma mpeleke madai yenu kwa wakati ili wayahakiki mapema,” alisema.

Katika mkutano huo, Waziri Ummy alibaini kwamba tatizo hilo haliko kwa watoa huduma bali NHIF kutokana na CCBRT kueleza kuwa madai ya mwezi uliopita yameshapelekwa NHIF.

“Kumbe tatizo liko kwetu NHIF. Nawaelekeza tusiwe kikwazo cha huduma bora kwa sababu mtoa huduma anategemea hizi fedha kulipa mishahara, kununua vifaa, kulipa umeme na maji. Tunataka watu waone raha ya kuwa na NHIF, sitaki mwisho wa siku watoa huduma waseme hatuzipokei bima kwa sababu malipo hawayapati kwa wakati,” alisisitiza.

Waziri Ummy pia aliwataka Watanzania waone umuhimu wa kuwa na bima kwa sababu ndiyo njia rahisi ya kupata huduma bila kikwazo cha fedha.

Alisema alikutana na kijana ambaye analipa fedha taslimu Sh. 50,000 ili kumwona daktari, gharama ambayo haihusishi vipimo na dawa.

“Nimemwambia NHIF kwa watu sita ni Sh. milioni 1.5, ukiigawa ni kama 250,000 kwa hiyo sisi tumeangalia mkiwa watu sita hawawezi kuumwa wote, kwa hiyo tunakamilisha utaratibu tuwe na bima ya afya ya mtu mmoja mmoja ili kila mtu ajipimie kifurushi chake,” alisema.

Alisema ndani ya wiki tatu, serikali itatangaza vifurushi vya mtu mmoja mmoja ambavyo vitawezesha Watanzania kupata huduma bora za afya.

Kuhusu kliniki hiyo kwa wagonjwa wa nje, alisema hata hospitali za serikali wamezielekeza iziweke ili kusaidia kujiendesha.

Pia alisema katika bajeti ya mwaka jana walihakikisha wanapunguza tozo kwenye vifaa tiba vinavyotolewa kwa msaada.

“Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) nimeshawaelekeza kuwa wapunguze tozo kwenye vifaa tiba vinavyoletwa na kliniki binafsi na hospitali binafsi, kwa sababu hii si biashara. Tutatoa taarifa kabla ya mwezi mmoja kuonyesha ni tozo gani za kupunguza kwenye vifaa tiba, dawa na vitenganishi,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Ummy alisema wagonjwa wa fistula wamepungua kwa sababu serikali imeviboresha vituo vya afya 350 ambavyo sasa vinatoa huduma bora za uzazi.

Pia alisema serikali imefanikiwa kupunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 40 kuanzia mwaka 2012 hadi 2018.

Awali, Msangi alisema malengo ya kuanzisha huduma hiyo kwa wagonjwa wa nje ni kwa sababu hawataki kutegemea wafadhili.

“Ukija kutibiwa katika huduma hii ya binafsi ujue utaokoa maisha ya watu wengi ambao hawana uwezo,” alisema.

Nesia Mahenge kutoka Shirika la Kuhudumia Watu wenye Ulemavu (CBM), aliiomba CCBRT ifike mikoa mingi Tanzania ili wagonjwa wasisafiri umbali mrefu kutafuta huduma.

Habari Kubwa