Waziri aibua uozo unaoua mashirika

07Dec 2021
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri aibua uozo unaoua mashirika

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amefichua uozo unaochangia mashirika mengi ya umma kufeli katika utendaji.

Amefichua sababu kubwa inayochangia ni bodi za mashirika hayo kutanguliza maslahi binafsi na kwamba ndio maana bodi nyingi zinavunjwa.

Kwamba zinavunjwa kutokana na kushindwa kusimamia ununuzi, maslahi binafsi pamoja na kuendekeza urafiki.

Amesema bodi nyingi zilishindwa kutimiza majukumu waliyopewa kutokana na baadhi ya maofisa watendaji wakuu wa mashirika kuwashika wajumbe wa bodi, hali inayosababisha kila jambo wanalopelekewa kulipitisha pasipo kuhoji.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizundua Bodi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), huku akiwatahadharisha wajumbe hao kuwa makini katika utendaji kazi wao, vinginevyo hawatadumu muda mrefu.

Alisema wajumbe wa bodi wengi wanakuwa na ‘personal interest’ (maslahi binafsi) hali inayowasababishia kujisahau kutimiza majukumu waliyopewa.

“Nikiona mtu anazembea namnyofoa namweka mwingine, hivyo hivyo hadi mambo yatakapokaa sawa. Wajumbe wengi wa bodi wanashindwa kusimamia majukumu yao, wanakuwa sehemu ya uongozi wa shirika,” alisema Prof. Mabarawa na kuongeza:

“Mkiacha urafiki na mtu mtafanikiwa. Nendeni mkalisimamie shirika, Ma-C.E.O (maofisa watendaji wakuu) wanatabia ya kuwashika wajumbe wa bodi, muwe na tabia ya kuuliza kila kitu siyo kila mnacholetewa mnakipitisha.”

Prof. Mbarawa alisema watu wengi wanafurahi wanapoteuliwa kuwa wajumbe katika bodi kwa sababu wanafahamu ni sehemu ya kukaa na kupata pesa.

“Bodi ni sehemu ya kumsaidia waziri na taasisi kutimiza malengo, lakini wengi wanakuwa na maslahi binafsi. Bodi ya ATCL mnakazi kubwa, manunuzi ni makubwa sana ATCL nendeni mkalisimamie hilo, jengeni tabia ya kuuliza, tukifanya hivyo kila mtu atakuwa salama, familia zenu zitakuwa salama.”

Kadhalika, Prof. Mbarawa aliwataka wajumbe wa bodi hiyo kuhakikisha ATCL inakuwa pamoja na kuzisimamia ndege zijiendesha kwa faida.

Aliwataka wajumbe hao kuhakikisha ATCL inakwenda kwenye soko la ushindani pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja.

“Soko la ATCL bado halikajaa vizuri, hivyo ni kazi yenu kuisukuma menejimenti. Baada ya miaka miwili tutakuwa na ndege zaidi ya 17 ni jukumu lenu kuzisimamia ndege hizo,” alisema Prof. Mbarawa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Profesa Neema Mori, alisema: “Tutatimiza matakwa na malengo ya wateja wetu, pia tutahakikisha ATCL inakwenda katika malengo yaliyopangwa. ATCL kuwa shirika la mfano, bora, pamoja na kutoa huduma zinazokidhi viwango.”

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, alisema kwa sasa shirika hilo linaingia katika ushindani wa kibiashara na mashirika mengine ya ndege.

Alisema kwa sasa imeboresha huduma za usafiri na imejipanga kufika katika miji mingi zaidi barani Afrika na nje ya Afrika.

Habari Kubwa