Waziri aipa maagizo nane Tume Madini

19Feb 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Waziri aipa maagizo nane Tume Madini

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko, ametoa maagizo manane kwa Tume ya Madini nchini, huku akionyesha namna serikali ilivyopata hasara ya mabilioni ya shilingi kutokana na wamiliki wa leseni kutolipa malipo stahiki ya serikali.

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko, picha mtandao

Maagizo hayo aliyatoa jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuwaendeleza na kuwasaidia wachimbaji wadogo, kuimarisha utoaji na usimamizi wa leseni za madini nchini.

Alisema kuanzia Januari 2019, wizara ilifanya uhakiki wa leseni zote za uchimbaji madini ambazo zimetolewa na kubaini leseni nyingi zimekiuka matakwa ya kisheria.

Alieleza kuwa kuna watu wamehodhi na kushindwa kuendeleza maeneo ya utafiti waliyopewa kinyume cha kifungu cha 36(1) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake, hivyo kusababisha wachimbaji wengine hasa wadogo kukosa maeneo ya kuchimba.

“Pia kushindwa kulipa malipo stahiki ya serikali ikiwa ni pamoja na ada ya mwaka kinyume na kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017,” alisema.

MADENI YA MABILIONI

Biteko alisema hadi kufikia mwezi huu, jumla ya leseni 18,341 kati ya 30,937 zinadaiwa Sh. bilioni 116.67 na kuagiza tume hiyo kuziandikia hati za makosa na zilipe fedha hizo ndani ya siku 30.

“Na kama wakishindwa kulipa madeni hayo ndani ya muda huo leseni hizo zifutwe ndani ya siku saba baada ya mwisho wa hati za makosa kwa mujibu wa kifungu cha 63 cha Sheria ya Madini,” alisema.

Aliongeza: “Katika zoezi hili lisiangalie nani anamiliki leseni hiyo hata kama taasisi ya serikali, hata ile leseni ya Liganga na Mchuchuma ambayo inamilikiwa na NDC na mbia wake na najua inadaiwa ada Dola za Marekani zaidi ya 375,000 sheria ifuate mkondo wake.”

Alifafanua kuwa katika madeni hayo leseni kubwa za utafiti(PL) zinadaiwa Sh. bilioni 61.67, leseni za uchimbaji mkubwa (SML) Sh. bilioni 6.41, uchimbaji wa kati (ML) Sh. bilioni 28.28 na uchimbaji mdogo (PML) Sh. bilioni 19.51.

LESENI KUFUTWA

Waziri Biteko alisema leseni za utafiti 110 na leseni za uchimbaji wa kati 52 zilikuwa zimeshapewa hati ya makosa zifutwe ndani ya siku saba.

“Na ziandikiwe hati ya madai mara moja na wakishindwa kulipa madeni hayo ndani ya siku 30 wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kifungu cha 93 cha Sheria ya Madini,” alisema.

Pamoja na hayo, Biteko aliiagiza tume hiyo kufuta leseni zote za utafiti ambazo zipo hai na hazina madeni, lakini toka zitolewe imepita miezi mitatu bila kuanza kuandaa na kukusanya vifaa stahiki kwa ajili ya utafiti.

“Pia miezi zaidi ya sita imepita bila kuanza utafiti kwa kuwa ni kinyume cha kifungu cha 36(1) cha sheria,” alisema.

WATENDAJI WATUMBULIWA

Kadhalika, aliagiza kusimamishwa kazi watumishi watano wa wizara hiyo kwa makosa mbalimbali ikiwamo kutoa leseni za uchimbaji mdogo kwa raia wa kigeni na kubadilisha leseni za maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuwapatia wakubwa.

“Kuna baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo likiwamo la Melela lipo Mvomero Morogoro, yametolewa leseni bila kufuata taratibu za utoaji leseni,” alisema.

Aliwataja wanaosimamishwa kwa kosa hilo ni Hamis Komba, Lucy Kimaro na Bakari Shemsanga.

“Haiwezekani tutenge maeneo kwa wachimbaji wadogo wao wakafanye wanavyojisikia wao kwa tamaa zao,” alisema.

Pia alisema kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini kinakataza leseni ndogo za uchimbaji kutolewa kwa wageni.

“Leseni namba PML003227NZ, PML003387NZ, PML003427NZ zimetolewa kwa mtu ambaye ni raia wa Kenya, lakini pia maombi yake namba PML12823/NZ, PML13036/NZ, PML13066/NZ, PML14632/NZ, PML23158/NZ, PML23159/NZ, PML25398/NZ, PML25786/NZ na PML25789NZ yapo katika hatua mbalimbali ya kupatiwa leseni kinyume cha sheria,” alisema.

Aliagiza tume hiyo kuwachukulia hatua walioshiriki kutoa leseni hizo ambao ni Fredrick Massawe na Elias Azaria.

WACHIMBAJI WADOGO WADAIWA BIL.1.7/-

Biteko alisema kuna wachimbaji hasa wadogo wamejenga mitambo ya kuchenjua dhahabu bila kufuata utaratibu, ambapo hadi kufikia mwezi huu takribani mitambo 639 haina leseni na imesababisha hasara ya Sh. bilioni 1.76.

Alisema fedha hizo zinatokana na ada ya maombi na ada ya mwaka ya mitambo hiyo, na kuagiza tume hiyo kuhakikisha kuwa mitambo yote inapatiwa leseni ndani ya siku 30.

“Mitambo ambayo itakuwa haijapata leseni ndani ya muda huo haitaruhusiwa kuendelea kufanya kazi na wahusika wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

MARUFUKU KUTOA LESENI MPYA

Waziri Biteko alipiga marufuku utoaji leseni mpya kwa kampuni au mtu binafsi aliyepewa Hati ya Makosa na kushindwa kurekebisha makosa hayo kwa kuwa ni kinyume cha kifungu cha 31(b) cha Sheria ya Madini.

Aliagiza tume kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa nchini kutenga eneo moja kwa kila mkoa na kusimamia ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji madini ndani ya miezi mitatu.

Hata hivyo, aliwaasa wachimbaji hasa wadogo kuomba leseni katika maeneo yatakayoachwa wazi ili kujiepusha na uchimbaji usio rasmi.

“Pia rai yangu wahakikishe wanatafuta njia mbadala ya kuzuia mashimo yao kuanguka mfano zege na mabati ya chuma badala ya kutumia miti ili kutunza mazingira,” alisema.

“Baada ya mwaka mmoja hatutaruhusu tena magogo kutumika. Taarifa zote za leseni zinazodaiwa zinapatikana kwenye tovuti ya wizara na tume,” alisisitiza Biteko.

Habari Kubwa