Waziri aitaka NHC kutafakari bei ya nyumba

11Jan 2020
Munir Shemweta
Masasi
Nipashe
Waziri aitaka NHC kutafakari bei ya nyumba

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameitaka Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kupitia upya gharama za nyumba zake ilizojenga maeneo ya pembezoni kwa ajili ya kuziuza.

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, picha mtandao

Dk. Mabula alitoa kauli hiyo juzi wilayani hapa alipotembelea mradi wa nyumba 54 zilizojengwa na NHC akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mikoa ya kusini na kutembelea miradi inayofanywa na NHC katika maeneo mbalimbali nchini.

Alitoa kauli hiyo kutokana na kulalamikiwa na wabunge wa Masasi, Rashid Chuachua, na wa Lulindi, Jerome Bwanausi, kuwa pamoja na halmashauri kuhitaji nyumba kwa ajili ya watumishi, gharama zimekuwa kubwa kiasi cha halmashauri na wananchi kushindwa kuzinunua.

“Ni vizuri bodi ikae iangalia namna ya kupitia upya gharama za nyumba zote zilizoko maeneo ya pembezoni kama hizi za Masasi maana zikiachwa bila kununuliwa, itakuwa hasara,” alisema.

Dk. Mabula alisema hata kama nyumba hizo zilizojengwa kwa ajili ya kuuza hazitanunuliwa, NHC iangalie namna ya kuzipangisha na kueleza uhitaji wa nyumba katika eneo la Masasi upo na watumisi wa serikali wanahitaji kuishi maeneo rafiki.

Pia alizitaka halmashauri nchini kuitumia NHC kujenga miradi ya nyumba za watumishi kulingana na mahitaji ili kuepuka kujenga nyumba ambazo zinaweza zisinunuliwe.

Meneja Mawasiliano wa NHC, Muungano Saguya, alisema shirika lake liko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo uliokuwa umesimama kwa muda na kwamba takriban Sh. milioni 600 zitatumika kuukamilisha na kusisitiza kuwa ni imani yake katika miezi sita ujenzi utakamilika.

Kwa mujibu wa Saguya, bei inayolalamikiwa ya Sh. milioni 54 kwa nyumba moja inatokana na gharama kubwa iliyotumiwa na shirika kuzijenga na kubainisha kuwa NHC iko mbioni kuzipangisha baadhi ya nyumba ambazo wananchi wameonyesha nia ya kupanga.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mabula alizitembea wilaya za Nanyumbu na Tunduru na kukagua utendaji kazi katika sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya hizo.

Mabula kwenye ziara hizo, alibaini utunzaji mbovu wa kumbukumbu za majalada ya ardhi pamoja na kiasi kidogo cha makusanyo ya maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango.

Kutokana na kasi hiyo ndogo, aliziagiza halmashauri za Nanyumbu na Tunduru kuongeza kasi ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi sambamba na kuzingatia utunzaji majalada ya ardhi kwa kufuata taratibu ikiwamo kuwapo mawasiliano katika majalada hayo kutoka ofisa mmoja kwenda kwa mwingine.

Habari Kubwa