Waziri akerwa watalii kupokwa vinyago

15Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri akerwa watalii kupokwa vinyago

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, ameingilia kati sakata la watalii kuacha vinyago walivyonunua kwa kukosa vibali kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Katika hatua hiyo, Kanyasu ameiagiza TFS iangalie namna bora  ya kutatua tatizo hilo kwa vile limekuwa na taswira mbaya kwa nchi.

Hali hiyo imetokana na  malalamiko ya watalii wengi baada ya kulazimika kuacha  vinyago kwenye viwanja vya ndege walivyokuwa wamevinunua kwenye maduka mbalimbali nchini kwa sababu ya kukosa vibali hivyo.

Kanyasu alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa makao makuu ya TFC jijini Dar es Salaam.

Alisema  watalii wengi  hununua vinyago hivyo kwenye maduka mbalimbali nchini kama zawadi kupeleka nchini kwao lakini  wanapofika kwenye viwanja vya ndege baada ya kumaliza shughuli zao, hudaiwa vibali vya kusafirishia jambo ambalo huwalazimu kuviacha kutokana na usumbufu wanaoupata.

Naibu Waziri alisema limekuwa likiwafanya watalii wengi kuondoka nchini wakiwa wamekasirishwa kutokana na utaratibu huo kutokuwa wazi huku wakiamini kuwa wamedhulumiwa mali zao.

Alisema malalamiko hayo  si mazuri licha ya kuwa TFS nia yake ni njema ya kuhakikisha lazima kuwe na vibali ya kusafirishia vinyago hivyo kwa ajili uthibiti wa uharibifu wa misitu.

Kanyasu alisema lazima ifanye mazungumzo na taasisi zingine  ili kutatua kero hiyo ambayo imekuwa ikileta picha mbaya kwa watalii na sekta ya utalii kwa ujumla.

Alisema ni rahisi kumpoteza  mteja (mtalii) lakini huchukua hata zaidi ya miaka 10 kumrudisha mteja ambaye amepotezwa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, nia ya TFS ni njema katika kulinda misitu lakini tatizo linaloonekana ni kwamba hakuna mawasiliano kati ya TFS na taasisi zingine kuhusiana  na biashara ya vinyago.

Amesema TFS ni lazima ikae meza moja na wauzaji wa vinyago pamoja na taasisi za uhifadhi ili kutatua kero hiyo wanayokumbana nayo watalii.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, aliahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ili kuwaondolea usumbufu watalii wanaokuwa wamevinunua vinyago hivyo.

Alisema suala la udhibiti wa usafirishaji  vivyago liko kisheria lakini kutokana na tatizo hilo, atafanya mazungumzo na taasisi zingine ili kuona namna bora ya kutatua kero hiyo.

Habari Kubwa