Waziri akunwa kampuni kuinua vijana wakulima

17Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
KILOSA
Nipashe
Waziri akunwa kampuni kuinua vijana wakulima

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Anthony Mavunde, ameisifu kampuni ya mbolea ya Petrobena East Africa Ltd kwa kuhakikisha wakulima wa Tanzania, hususani vijana, wanapata maendeleo kupitia sekta ya kilimo.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Anthony Mavunde.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa mavuno ya mpunga katika shamba lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 50 la vijana wa Agri-Ajira, katika Kijiji cha Mambegwa wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, Naibu Waziri alisema mchango wa kampuni hiyo katika kuinua sekta ya kilimo ni mkubwa.

“Naipongeza sana kampuni hii chini ya uongozi wa Peter Kumalilwa kwa kutembea kwenye barabara ya malengo ya serikali. Mnatekeleza azma ya taifa ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025,” alieleza.

Mavunde alisema Tanzania haiwezi kufikia azma ya uchumi wa viwanda kama sekta ya kilimo haitafanyiwa mabadiliko makubwa, na kuongeza kwamba wadau wa kilimo, kama Petrobena lazima wajitoe na kuweka nguvu zao zote ili uzalishaji wa malighafi uwe mkubwa na wakutosheleza mahitaji ya viwanda nchini.

Amekisifu kikundi cha Agri-Ajira kwa kuwa na shamba zuri la mpunga.

“Hiki ni kielelezo kwamba vijana wakiaminiwa wanakuwa katika nafasi kubwa ya kuleta matokeo chanya nchini,” alisema Mavunde na kuongeza kuwa vijana hao wanatoa funzo kubwa kwa wahitimu wa vyuo nchini

ambao wamekuwa na changamoto kubwa katika kupata ajira.

Pia alitoa wito kwa vijana kuacha kusaka kazi na wengine

kuchagua kazi katika soko la ajira. Badala yake waitafsiri kwa vitendo elimu wanayoipata vyuoni ili wajijengee kipato na kuchangia pato la taifa.

Mkurugenzi wa Petrobena, Peter Kumalilwa, alimshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea shamba hilo na kusema kitendo hicho kitahamasisha vijana kupenda kilimo na kuchochea upatikanaji wa malighafi za viwanda.

“Tunakushuru waziri kwa kuungana na vijana hawa. Kitendo hiki kinawapa hamasa vijana hawa na pia kitawachochea vijana wengine nchini kuanza kuweka nguvu zao katika sekta ya kilimo ambayo ni kiunganishi muhimu kwa uchumi wa viwanda,” alisema Kumalilwa.

Kumalilwa alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, kwa kuwaongoza vijana hao ambao walihangaika kwa muda mrefu bila mafanikio.

“Tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa kutupatia eneo hili. Lakini pia jitihada zake ndizo zilizotengeneza mazingira ya Petrobena na Agri-Ajira kukutana na leo hii tunashuhudia tukio hili lenye kutia moyo vijana hawa baada ya kuhangaika kwa muda,” alieleza.

Samweli Kitila, mwanachama wa Agri-Ajira, alisema haikuwa kazi rahisi kufikia mafanikio hayo kwa sababu vijana wamekumbana na changamoto nyingi.

“Haikuwa kazi rahisi hata kidogo kuziacha shahada zetu na kuamini katika kufanya kazi, uzalendo na weledi mpaka pale tulipokutana na Petrobena East Africa ambao walibadili ndoto zetu na kuwa kitu halisi na kinachowezekana, hakika tunawashukuru sana,” alisema Kitila ambaye ni mhitimu wa shahada ya kwanza Chuo Kikuu Kilimo cha Sokoine (SUA).

Petrobena East Africa Ltd, msambazaji mkubwa wa mbolea ya YARA na imekuwa ikiwasaidia kifedha na elimu wakulima wadogo.