Waziri alalamika kutokabidhiwa viwanja alivyonunua

22May 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Waziri alalamika kutokabidhiwa viwanja alivyonunua

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amelalamika bungeni kutokabidhiwa viwanja viwili alivyonunua katika Jiji la Dodoma tangu mwaka 2018.

Amesema amefuatilia kwa muda mrefu viwanja hivyo, ikiwamo kumfuata Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge, na Mkurugenzi wa jiji hilo, Godwin Kunambi bila mafanikio.

Kutokana na kushindwa kuvipata viwanja hivyo, Waziri Kamwelwe alilazimika kumuomba Spika Job Ndugai kumsaidia ili aweze kuvipata, ingawa ameshavilipia.

Waziri Kamwele alilazimika kuyasema hayo baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Willum Lukuvi, kuwataka wabunge wanaohitaji viwanja kwa ajili ya kujenga makazi au nyumba za biashara wamuone na atawasaidia haraka.

Kwenye maelezo yake, Waziri Lukuvi alisema: “Jiji la Dodoma wamejitahidi sana, tumeuza viwanja 10,000. Hadi hapa ndani (bungeni) Naibu Waziri wangu alikuwa anagawa fomu hapa mwaka juzi, watu wamenunua viwanja viwili, vitatu,” alisema na kiuongeza:

“Wenye mawazo ya kujenga ‘Guest House’ (nyumba za wageni), apartments, nyumba za biashara. Hata anayetaka kiwanja aende Jiji, akikosa anione mimi, kuna viwanja vya kumwaga. Hapa ndiyo mahali pake, kwa viongozi kama nyie wabunge hapa ndiyo ‘second home’,” alisema Lukuvi.

Baada ya maelezo hayo ya Waziri Lukuvi, ndipo Waziri Kamwelwe alipoinuka na kusema:

“Mimi nilipewa ofa nikalipia viwanja viwili siku hiyo hiyo, shahidi yangu Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mavunde, mpaka leo sijapata kiwanja. Tena mimi ni waziri, nimeongea kwa Mkuu wa Mkoa, kwa Mkurugenzi, hadi leo sijapata kiwanja, nimelipa fedha zote,” alisema.

Spika Ndugai ilimlazimu kumweleza Waziri Kamwelwe kuwa atamsaidia kuhakikisha anapata viwanja hivyo.

Habari Kubwa