Waziri ampa kibano mkurugenzi malipo ya korosho

01Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Waziri ampa kibano mkurugenzi malipo ya korosho

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, ametoa siku 14 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CBP), Dk. Anslem Moshi, kukamilisha malipo ya wakulima wote waliouza korosho msimu wa mwaka 2018/19.

Hasunga alitoa agizo hilo jana alipotembelea na kukagua shughuli za utendaji kazi zinazofanywa na bodi hiyo jijini hapa.

Alisema bodi hiyo ilipewa dhamana ya kununua korosho mwaka 2018 kwa niaba ya serikali na tayari serikali imeshatoa fedha zote kwa ajili ya wakulima lakini haijakamilisha malipo, hivyo ni lazima itekeleze agizo hilo ndani ya siku hizo.

“Ndani ya siku 14 sitaki kusikia malalamiko ya wakulima. Lazima wakulima wote wawe wamelipwa fedha zao haraka iwezekanavyo,” alisisitiza.

Hasunga alimwagiza mkurugenzi huyo kuwasilisha haraka mpango kazi wa namna viwanda vitakavyofanya kazi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zitakazohitajika na wateja na kukidhi matarajio ya serikali ikiwa ni pamoja na kuainisha idadi ya watumishi wanaohitajika.

Hasunga aliiagiza kampuni ya Monaban ambayo ilikuwa imekodi kiwanda cha nafaka kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa mwaka jana ya kuhamisha mali zao zote zilizoko katika eneo hilo la serikali kwa kuwa kesi mahakamani na notisi ilishaisha.

Akiwa kiwandani hapo, Waziri Hasunga alibaini uchakavu wa mitambo iliyopo pamoja na uchache wa watumishi wanaofanya kazi, hivyo kuagiza kufanyika ukarabati wa majengo kuanzia mwezi huu badala ya Oktoba, mwaka huu, kama kampuni hiyo ilivyopanga.

“Tukisubiri mpaka mwezi wa kumi tutakuwa tumechelewa kwa kuwa mvua zitaanza kunyesha jambo ambalo litasababisha kushindikana kufanyika ukarabati,” alisema.

Hasunga alisema lengo la serikali ni kufufua viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya nafaka nchini ili kuzalisha bidhaa mbalimbali kama unga na kuuza katika masoko ya ushindani ndani na nje ya nchi.

Habari Kubwa