Waziri ampa mkandarasi maji siku 7

20Apr 2019
Happy Severine
MASWA
Nipashe
Waziri ampa mkandarasi maji siku 7

WAZIRI wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Pett Cooperation anayejenga chujio la mradi wa maji Zanzui, lililoko wilayani Maswa, mkoani Simiyu, kukamilisha na kukabidhi mradi huo ndani ya siku saba tofauti na hapo atafukuzwa kazi na kufunguliwa mashtaka.

WAZIRI wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.

 

Akizungumza jana baada ya kukagua ujenzi huo majira ya saa 1:30 usiku, Waziri Mbarawa alisema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa chujio hilo kwa sababu niwa siku nyingi na wenye kusuasua.

Alisema ni miaka minne sasa tangu uanze kujengwa mwaka 2015, wakati huo mkataba unaonyesha ulitakiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi tisa.

''Hii haikubaliki, wananchi wa hapa wanaugua magonjwa ya matumbo kwa sababu ya kunywa maji yasiyosafishwa...ikitokea kipundupindu athari yake ni kubwa na wananchi hawa wanataka wapate majisafi na salama kama eneo jingine la nchi yetu,'' alisema Waziri Mbarawa na kuongeza:

...lakini wewe, wewe kwa uzembe wako, kwa ukatili wako na kwa kutopenda nchi yetu umesababisha hili tatizo, una miradi zaidi ya 15 unayotekeleza hapa nchini na umekuwa ukipewa mradi huku na kule na kupeleka fedha kidogo pamoja na kuhonga ili upewe miradi, itakuwaje mtu mmoja upewe miradi mingi,'' alihoji.

Alimtaka Mkuu wa Kituo cha Polisi Maswa (OCD) kumweka mahabusu kwa saa mbili na baada ya hapo aandike maelezo vizuri ili kuhakikisha ifikapo Aprili 25, wananchi wa eneo hilo wanapata maji, huku akisisitiza kuwa ameshatoa fedha Sh. milioni 152.23 kwa ajili ya malipo yake na asipofanya hivyo atafungwa jela zaidi ya miaka miwili kwa kufanya utapeli wa miradi.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalaghe, alisema kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 92 pamoja na matamko ya viongozi mbalimbali, mkandarasi amekuwa akisuasua kukamilisha mradi huo.

Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Maswa (Mwauwasa), Archades Anaclet, alisema mradi huo ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2015, licha ya mradi kukabiliwa na changamoto ya malipo, lakini aliongezewa muda wa utekelezaji.

Aliongeza kuwa mkandarasi aliwahakikishia angekamilisha shughuli zote mwezi Desemba, mwaka jana na kukabidhi mradi, lakini hadi leo hajakamilisha, huku akiendelea kuwahakikishia atakabidhi mradi huo Aprili 30, mwaka huu.

Kwa upande wake mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Pett Cooperation, Tryphone Elias, alisema changamoto za kucheleweshewa hati za malipo zimesababisha kuongezewa muda wa ujenzi, hali iliyofanya kupanda kwa bei ya bidhaa zinazotakiwa katika mradi huo.

Mradi umelenga kunufaisha wakazi zaidi ya 17,000.

Habari Kubwa