Waziri amulika gharama upimaji saratani

25Jan 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Waziri amulika gharama upimaji saratani

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameagiza Hospitali ya Benjamin Mkapa kupunguza gharama za kuchunguza saratani ya matiti kwa wanawake kutoka Sh. 70,000 hadi 30,0000 kama ilivyo kwa hospitali zingine za taifa.

Pia, ameitaka hospitali hiyo kujiunga na tiba mtandao ili kutoa tiba kwa wagonjwa kwa haraka na kwa ufanisi na kuwapunguzia wagonjwa muda wa kusubiri majibu hususani ya mionzi.

Aliitoa maagizo hayo jana alipotembelea hospitali hiyo kujionea hali ya utoaji huduma.

Alisema ni vyema wakajiunga na huduma ya tiba mtandao ili kutoa huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

"Mnatakiwa mkajifunze huduma hii kutoka Hospitali ya Muhimbili au MOI," alisema.

Waziri huyo alisema hivi sasa kwenye hospitali nyingi kuna shida ya wataalamu wa kusoma picha kwa kuwa wataalamu wengi waliopo ni wale wa kupiga.

"Tunao wataalamu wengi wa kupiga picha maana kwenye mionzi kuna aina mbili za wataalamu wapo wa kupiga picha (radiographer) na wa kusoma picha, hivyo serikali itahakikisha inapata wataalamu wengi zaidi wa kusoma ili kukidhi mahitaji," aliahidi.

Waziri Ummy alisema wizara ina lengo la kuziunganisha hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya kwenye mfumo wa hospitali za rufaa za mikoa kwa kufunga senta zitakazosaidia hospitali za wilaya na vituo vya afya vinavyofanya vipimo vya ‘utra sound’ na ‘x-ray’ na majibu yakasomwa haraka na wataalamu wa hospitali za rufaa na kutoa majibu haraka bila kumsubirisha mgonjwa kwa muda mrefu.

Alitoa wito kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani kutosafiri hadi Dar es salaam kupata huduma za kibingwa kwa kuwa huduma zote karibu zinapatikana hapo na wizara itapeleka madaktari bingwa wa mishipa ya fahamu na mifupa.

Habari Kubwa