Waziri anusa ufisadi mradi Waziri anusa ufisadi mradi wa maji maji

21Feb 2020
Dege Masoli
Mkinga
Nipashe
Waziri anusa ufisadi mradi Waziri anusa ufisadi mradi wa maji maji

NAIBU ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameagiza kuchunguzwa ujenzi wa mradi wa chanzo cha Maji cha Mbuta katika kata Mwakijembe wilayani Mkinga kwa kile alichobaini kuwapo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh. milioni 400 ambazo licha ya kutumika lakini hakuna kazi iliyofanyika.

NAIBU ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, picha mtandao

Aweso alitoa agizo hilo juzi alipokuwa kwenye ziara ya siku moja wilayani hapa kutembelea miradi ya maji. Baada ya kufika kwenye mradi wa maji wa Mbuta unaotekelezwa kwa gharama ya Sh. bilioni 1.7, hakuridhishwa na matumizi ya Sh. milioni 400 zilizodaiwa kutumika kuchimba bwawa.

Kutokana na kutilia wasiwasi matumizi ya fedha hizo, aliagiza kuundwa timu ya uchunguzi wa matumizi ya fedha hizo akiwamo mkandarasi wa mradi, Kampuni ya White City pamoja na kamati iliyohusika kwenye utekelezaji huo.

Pia aliagiza kukamatwa kwa msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Castory Kenneth, kwa kile alichodai kutokuwa makini kusimamia wajibu wake na kusababisha matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Naibu Waziri pia alihoji ulazima wa watekelezaji wa mradi huo kuanza kujenga matangi na kusambaza mabomba badala ya kushughulikia chanzo cha maji kwanza jambo alilodai ni kukosa uadilifu na kutaka kupata asilimia 10.

"Hawa mabwana najua walikimbilia kusambaza mabomba na kujenga matangi kwa kuwa huko ndipo kwenye asilimia 10 ya haraka, vinginevyo wangeelekeza nguvu kutengeneza chanzo kabla ya kazi waliyoifanya," alisema Aweso.

Hata hivyo, Aweso alipongeza mradi wa maji wa Mwakijembe kutokana na kile alichokieleza mwonekano unaolingana na thamani ya fedha baada ya kuelezwa kuwa ujenzi wa chanzo hicho umegharimu zaidi ya Sh. milioni 200 huku matumaini ya kazi hiyo yakionekana.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara hiyo, Aweso aliwataka wataalamu kubadilika na kutumia elimu yao kwa faida ya wananchi na taifa kwa ujumla na kwamba utendaji kazi wa ujanjaujanja hautawasaidia.

Alisema wataalamu ndio tegemeo kubwa la serikali na kwamba wasitumie ugumu wa mazingira ikiwamo miundombinu kama sehemu ya kula fedha za miradi zinazotolewa na serikali au wafadhili kwa kuwa hawatakuwa salama
kwa kufanya hivyo.

Naibu Waziri alisema wananchi wana matatizo mbalimbali ya ukosefu wa maji na wanataka huduma hiyo huku akisisitiza kuwa serikali imekusudia kuwaondolea changamoto hiyo wananchi, hivyo wataalamu wasiwe vikwazo.

Habari Kubwa