Waziri anusa ufisadi Tarura

28Feb 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri anusa ufisadi Tarura
  • *Ampa siku 7 mkurugenzi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amemtaka Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Abdul Digaga, kuwasilisha taarifa za makusanyo ya mapato ya halmashauri na majiji yote nchini ndani ya siku saba kuanzia jana.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, picha mtandao

Alitoa agizo hilo jana baada ya kufanya ziara katika Ofisi za Tarura Mkoa wa Dar es Salaam na kubaini kuwapo kwa upotevu wa zaidi ya Sh. milioni 200 zilizotakiwa kukusanywa na Tarura katika jiji hilo ndani ya siku sita, lakini zilikusanywa Sh. milioni 24 pekee.

Jafo pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Joseph Nyamhanga, kufuatilia kwa karibu suala hilo na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa Idara ya Ununuzi ya Tarura kutokana na uzembe huo.

Waziri huyo alisema fedha hizo zilipaswa kukusanywa kuanzia Februari Mosi hadi 6, mwaka huu na kwa wastani, kila siku walipaswa kukusanya Sh. milioni 39 (Sh. milioni 234 kwa siku sita), lakini katika kipindi hicho cha siku sita, Tarura walikusanya Sh. milioni 24 pekee.

"Huu ni uzembe wa hali ya juu, kwa siku sita Tarura mmepoteza zaidi ya Sh. milioni 200, ambazo mlipaswa mzikusanye kwenye maegesho ya magari," alisema.

Jafo aliongeza: "Namwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tarura awasiliane na Katibu Mkuu Tamisemi asimamie jambo hili kwa sababu utendaji kazi wa Idara ya Ununuzi ya Tarura hauko vizuri, wahakikishe wanafanya uamuzi sahihi kwanini Tarura inaharibu."

Alisema tatizo linaonekana kuwapo katika idara ya ununuzi ambayo imezembea kuagiza mashine (POS) zinazotumika kutoa risiti za wanaoegesha magari ili walipe fedha.

"Kwa sababu hapahapa mlifanya manunuzi na mlitangaza mzabuni wenyewe, baadaye mkaingiwa na mashaka sana, mkaamua kutangaza tenda na kwa sababu ya ubabaishaji mwingi, mkaamua kufuta tenda, ina maana mlifanya hivyo kwa makusudi ili kukosekana kwa mapato haya, ukiangalia upande wa manunuzi, una matatizo sana," Jafo alisema.

Alisema kwa sababu tatizo lipo kwenye idara ya ununuzi na wamekaa kimya hadi hapo alipowatembelea, Jafo alisema anahitaji kupata taarifa za makusanyo katika halmashauri na majiji yote.

"Lengo kubwa la kutaka taarifa hizi ni kuzuia upungufu wa aina yoyote Tarura na Katibu Mkuu afanyie kazi upungufu uliopo na kuchukua uamuzi sahihi, kwa sababu nafahamu Tarura wanafanya kazi nzuri maeneo mengine," alisema.

Alisema ana taarifa za kuwapo kwa manispaa nyingine ambazo hazikusanyi kabisa fedha hizo na hazisimamiwi, hivyo kuna haja apewe taarifa za makusanyo ili kufanyia kazi suala hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Tarura, Francis Mwasota, alisema sababu ya kutokusanya mapato hayo ni mzabuni aliyepewa tenda, M/S Climate kushindwa kuwasilisha POS 1,500 kwa wakati kwa mujibu wa mkataba waliongia na Tarura.

Alisema kulikuwa na ucheleweshaji wa upatikanaji wa POS kutokana na mkandarasi kutokamilisha taratibu zilizotakiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) ili watoe kibali cha kuagiza POS.

Alisema kuanzia Februari Mosi, mwaka huu, Tarura iliingia mkataba na watoa huduma wa kutoza ada ya maegesho kwa kuzingatia mgawanyo wa kanda mbili za Manispaa za Kinondoni na Ubungo na kanda ya pili inayojumuisha Manispaa za Ilala, Temeke na Kigamboni.

Alisema jumla ya Sh. milioni 366.3 katika kipindi cha kuanzia Februari 6 hadi 25, mwaka huu, zikiwamo za kanda ya Kinondoni na Ubungo, Sh. milioni 109.57 na Ilala, Temeke na Kigamboni Sh. milioni 256.73 zilikusanywa.

Habari Kubwa