Waziri ashindwa mtihani wa JPM

27Jan 2017
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri ashindwa mtihani wa JPM

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene jana alishindwa kutaja faida ambayo imepatikana tangu kuanza kwa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (Dart) Mei, mwaka jana.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.

Akizundua mradi huo juzi jijini, Rais John Magufuli aliwapa saa tano Simbachawene na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

“Ifikapo leo jioni hawa mawaziri wawili na viongozi wa Dart wanieleze mradi huu umetengeneza faida kiasi gani, lazima wananchi wajue fedha wanazolipa zinakwenda serikalini au mifukoni mwa watu,” alisema Rais Magufuli.

Lakini jana, Simbachawene alishindwa kutaja faida iliyotengenezwa na Dart katika miezi nane ya ukodishaji wa miundombinu hiyo kwa kampuni ya Udart, katika mkutano na waandishi wa habari, na badala yake akataja tu mapato.

Awamu ya kwanza kati ya sita za mradi huo, imegharimu Sh. bilioni 403.

Miundombinu ya mradi huo ilianza kujengwa 2010 na kuchukua miaka mitano kukamilika, kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Simbachawene alisema tangu Mei, mwaka jana, zimekusanywa Sh. bilioni 19 na kwamba makusanyo kila mwezi yamekuwa yakiongezeka na kumekuwa na faida kutokana na uendeshaji wa mradi huo.

Waziri Simbachawene alisema mradi huo kwa mwezi Mei ulianza kwa kukusanya Sh. milioni 800.

Alisema makusanyo hayo yalipanda hadi kufikia Sh. bilioni moja hadi Sh. bilioni mbili na kwamba kwa Novemba na Desemba, mwaka jana, yalifikia Sh. bilioni tatu.

“Makusanyo tangu mradi uanze, kumekuwa na faida kubwa na hakuna hasara,” alisema Simbachawene bila kutaja gharama za uendeshaji ili kuonyesha kama ni ndogo kuliko mapato.

Alisema ili kujua faida iliyopatikana ni lazima kufanyike hesabu kutokana na kuwapo kwa gharama za uendeshaji kama vile mafuta, uendeshaji, mishahara, taasisi mbalimbali ambao ni wadau na msimamizi wa miundombinu ambaye ni Dart.

Aidha alisema gharama nyingine ni mkusanyaji wa mapato (Max-Malipo), meneja aliyetoa fedha ambaye ni Benki ya NMB, ulinzi, usafi, umeme na maji.

Simbachawene alisema kwa kutoa gharama hizo ndipo itapatikana faida na kuongeza kuwa Dart inalipwa Sh. milioni 8.1 kila siku kutoka katika makusanyo yanayopatikana.

Alisema awali Dart ilikuwa inalipwa Sh. milioni 4.4.

“Sasa kama kila siku Dart wanalipwa Sh. milioni 8.1 kwa mwezi watakuwa wanapata Sh. milioni 200 na wakaweza kulipia gharama zote ikiwamo kodi ya pango, maji, umeme na mishahara, hivyo huwezi kusema kuna hasara,” alisema.

Awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya BRT yenye urefu wa km 20.9 inajumuisha barabara ya Kimara–Kivukoni, Magomeni-Morocco na Fire–Kariakoo.

Huduma ya mabasi katika awamu ya kwanza inatolewa katika njia nane, vituo vikuu vitano, vituo vidogo 28 na karakana moja.

Huduma hiyo inatolewa na mabasi 140 yanayojumuisha mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja na mabasi madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.

Imeandikwa na Gwamaka Alipipi na John Simwanza

Habari Kubwa