Waziri ashtukia maofisa wake kupandishana vyeo 

15Mar 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Waziri ashtukia maofisa wake kupandishana vyeo 

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema ana taarifa za baadhi ya watendaji wa wizara hiyo kupandishana vyeo kiholela kutokana na kujuana.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, picha mtandao

Kutokana na changamoto hiyo, waziri huyo amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dorothy Mwanyika, kuhakikisha watendaji wa wizara hiyo wanapewa nafasi za kuongoza kwa uwezo wao na si upendeleo kama ilivyokuwa awali.Lukuvi aliagiza kufanyika kwa mchujo wa watendaji wa wizara hiyo kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakiipa sifa mbaya wizara kutokana na kujihusisha na rushwa na kuonea wananchi.

Lukuvi alifichua changamoto hiyo jana jijini Dodoma alipofungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichojadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 na mwelekeo wa bajeti ya mwaka huu wa fedha (2019/20).


Alisema kuna vijana wengi wenye uwezo, lakini wanaminywa na kunyimwa nafasi hizo kutokana na mafaili yao kuonekana "ni mepesi na hawana uzoefu kazini".


"Matokeo yake, wizara inakosa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana kuwa na viongozi wasio na tija wala sifa ya kutekeleza majukumu husika. Siwezi kukubali mtu anasukumiwa jalada wakati mtu hana uwezo, halafu yeye anapitisha na kumpa mtu cheo," alisema.

Lukuvi aliagiza kuwa kufikia Julai 7, mwaka huu, watumishi wote kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, wawe chini ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

"Nakuagiza Katibu Mkuu kupanga upya watumishi kwa mujibu wa uwezo wao na sifa ya kusimamia shughuli za wizara, ili kila mtu anayestahili aongoze, siyo kwa kujuana kama ilivyokuwa ikifanyika hapo zamani, mtu kupewa cheo lazima kujuana," alisema.

Lukuvi: "Nina taarifa za mtumishi ambaye ana uwezo mkubwa, lakini mmempiga teke mara zote, kila nafasi aliyostahili amenyimwa, lakini hivi sasa ameshastaafu, ndiyo katibu mkuu anasema amegundua ana sifa.

"Sasa mnataka mumrudishe kwa mkataba, sasa ndiyo mmejua ana uwezo baada ya kustaafu? Nimeshangazwa sana."

Lukuvi alitoa miezi miwili hadi Mei 30, mwaka huu, watendaji wa wizara hiyo wawe wamekusanya kodi kwa wadaiwa wote wa kila kanda na kila wilaya kwa mujibu wa watu waliowasajili na wanaomiliki ardhi katika maeneo hayo.

Alisema katika eneo hilo, anataka wafanye marekebisho na marejeo kwa kuingiza takwimu sahihi katika mitandao yao na kila wilaya lazima watu wote waliomilikishwa watambulike kwenye mfumo.

Waziri huyo pia alisema bado kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuendelea kuwapo kwa mchezo mchafu wa kuficha mafaili katika ofisi ya msajili na sehemu nyingine.