Waziri ashtukia tena balaa mifuko plastiki

14Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Waziri ashtukia tena balaa mifuko plastiki

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene, amewaonya wafanyabiashara wanaoingiza mifuko mbadala isiyokidhi viwango.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene, picha mtandao

Pia, amewaonya wamiliki wa viwanda vinavyozalisha mifuko laini ya plastiki kwa kificho na kuiingiza sokoni kwa magendo kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma jana, Simbachawene alisema pamoja katazo la mifuko ya plastiki kuibua fursa za kuwekeza katika kuzalisha mifuko mbadala, wapo baadhi ya watu wanaingiza na kuzalisha mifuko mbadala aina ya non-woven ambayo haikidhi mwongozo wa viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango (TBS).

Aliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), TBS kwa kushirikiana na kikosi kazi cha kitaifa cha katazo la mifuko ya plastiki, kufanya ufuatiliaji na kuwabaini wazalishaji hao na hatua zichukuliwe dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuteketeza bidhaa hizo ili iwe fundisho kwa wengine.

Waziri huyo alisema wapo baadhi watu wanageuza matumizi ya vifungashio vya mifuko laini ya plastiki (plastic tubings) kama vibebeo vya bidhaa mbalimbali kama vile nyanya, karoti, njegere pamoja na uingizaji wa magazeti yaliyotumika kwa ajili ya kufungashia bidhaa katika maeneo ya masoko, maduka na maeneo mengine ya biashara.

“Hali hii ni makosa kisheria, hivyo naelekeza NEMC, TBS pamoja na kikosi-kazi cha kitaifa washirikiane kwa karibu na kamati za ulinzi na usalama za mikoa, wilaya na mitaa nchini, kuendelea kufanya kazi bila kuonea mtu yeyote katika kudhibiti matumizi ya mifuko mbadala aina ya non-woven na kudhibiti uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya non-woven isiyokidhi vigezo vinavyokubalika kisheria,” alisema.

Simbachawene alibainisha kuwa NEMC kwa kushirikiana na TBS wameendesha ukaguzi katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata mifuko ya Non-Woven isiyokidhi viwango zaidi ya vipande milioni mbili na rollers zaidi ya 200 kwa ajili ya kutengeneza mifuko hiyo na kwamba mifuko hiyo imezuiliwa kuingia sokoni na hatua za kisheria zinaendelea.

Aliongeza kuwa mifuko laini ya plastiki (plastic tubings) vipande 9,600 vimekamatwa Mwanza zikiwa kwenye magunia manane ambayo na akapongeza juhudi zinazofanywa na mamlaka mbalimbali za serikali ikiwamo NEMC, TBS na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti wimbi la uingizaji wa mifuko hiyo isiyokidhi viwango.

Habari Kubwa