Waziri atahadharisha tishio ongezeko la watu uhifadhi

05Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
 MWANZA
Nipashe
Waziri atahadharisha tishio ongezeko la watu uhifadhi

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, ametahadharisha kuhusu ongezeko la watu nchini, akitaka mikakati kabambe kuhakikisha hifadhi za taifa na maeneo tengefu yanalindwa dhidi ya tishio hilo.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla.

Dk. Kigwangalla aliyasema hayo jana jijini Mwanza alipofungua mkutano wa mwaka wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na wahariri na waandishi waandamizi nchini.

Katika mkutano huo uliokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Tanapa, waziri huyo alisema ustawi wa uhifadhi uko hatarini kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ongezeko la watu.

Alisema idadi ya watu Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa kati ya milioni 50 na 60, lakini katika miaka 10 ijayo, idadi hiyo inatarajiwa kufikia watu milioni 100, hivyo akashauri kuwe na mikakati ya kulinda hifadhi dhidi ya uvamizi.

“Baada ya miaka 50 ijayo, idadi ya watu nchini inatarajiwa kuwa zaidi ya milioni 200, lakini ardhi inabaki kuwa ile ile. Hii ni changamoto kwa sababu presha itakuwa kubwa kwenye maeneo ya hifadhi na ikolojia kwa sababu ardhi haitatosha watu wote.

“Sasa, kwa kuzingatia hilo, ni lazima tulinde hifadhi zetu ili ziendelee kuchangia uchumi wa nchi kwa kuingiza fedha za kigeni, hifadhi zetu pia ni chanzo cha hewa muhimu kwa maana ya oksijeni, maji na hata mbao.

“Lazima tuhakikishe usalama wa taifa letu unakuwapo na jambo hili sharti tuliwekee mikakati leo maana Tanzania bila hifadhi, haiwezi kuwa na hadhi iliyonayo kwa sasa kiuchumi.

“Tusiangalie maslahi yetu tu sisi tuliopo kwa sasa, tuache ubinafsi, tuchukue hatua kwa pamoja kuhakikisha hifadhi zetu zinaendelea kuwapo kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho,” Dk. Kigwangalla alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa sekta ya utalii na uhifadhi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, akibainisha kuwa kwa sasa inachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni na imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 600,000 na zisizo rasmi zaidi ya milioni mbili.

Alisema wabunge wengi kwa sasa ‘wanalia’ na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, lakini katika miaka 50 ijayo, watunga sera hao hawatalilia maji kwa ajili hiyo, bali wataibana serikali kuhusu upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Dk. Kigwangalla aliipongeza Tanapa kwa kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo ya ujenzi wa shule, zahanati na vituo vya afya kwa lengo la kusaidia jamii, akieleza kuwa suala hilo litaongeza hamasa kwa wananchi kushiriki katika ulinzi wa hifadhi.

Dk. Kigwangalla pia alitumia mkutano huo kumshukuru Rais John Magufuli kwa kukubali kushiriki uzinduzi wa hifadhi mpya ya taifa utakaofanyika Jumanne mkoani Kagera.

Kamishna wa Tanapa, Dk. Allan Kijazi, alisema wamekuwa wakiitumia mikutano hiyo ya kila mwaka na wahariri na waandishi wa habari waandamizi kupata mrejesho na kufanya maboresho katika sekta ya utalii na uhifadhi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, aliipongeza Tanapa kwa kupeleka mkutano huo mkoani mwake na kuishauri kuishiriki mikoa na wilaya katika kuhamasisha utalii na ulinzi wa hifadhi nchini.