Waziri ataka hatua kwa watumishi wanaoishi mjini

19Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Geita
Nipashe Jumapili
Waziri ataka hatua kwa watumishi wanaoishi mjini

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, kusimamia maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ya kuhakikisha watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanaoishi mjini Geita-

-wanahamia maeneo ya jirani na vituo vyao vya kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mchengerwa alitoa maelekezo hayo jana katika kijiji cha Kakubilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Geita.

Alisema kuwa Waziri Mkuu alikwishatoa maelekezo ya watumishi wote wanaofanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuishi katika vituo vyao vya kazi lakini bado kuna watumishi wanaishi mjini Geita, jambo ambalo linaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Pamoja na maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu, nimepata taarifa kuwa kuna watumishi bado wanaishi Geita mjini na sio kwenye vituo vyao vya kazi huku wakitumia gharama za serikali kuwafikisha kwenye vituo vyao vya kazi kila siku,” alisema.

Katika kuhakikisha maelekezo ya Waziri Mkuu yanatekelezwa kikamilifu, Mchengerwa alitoa wiki mbili kwa watumishi wote wa halmashauri hiyo wanaoishi mjini Geita kuhamishia makazi yao kwenye maeneo wanayofanyia kazi.

Mchengerwa alisema kuwa anatarajia ndani ya wiki mbili alizozitoa, watumishi wote wanaoishi mjini watakuwa wamehamia karibu na maeneo wanayotoa huduma kwa wananchi na kwa kuwa ana vyanzo vingi vya kupata taarifa, hatosita kuchukua hatua kwa watakaokaidi.

Alisema yeye ni mlezi wa watumishi wa umma, hivyo amelazimika kwenda wilayani Geita ili kuhakikisha maelekezo ya Waziri Mkuu yanatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Waziri huyo pia alikagua Zahanati ya Kakubilo iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF na kuwaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwa ofisi yake itahakikisha inapeleka watumishi watakaotosheleza kutoa huduma kwa wananchi.

Mchengerwa alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Geita kwa kuhimiza watumishi kuishi katika maeneo wanayofanyia kazi ili wawe na tija katika utoaji wa huduma kwa umma.

Habari Kubwa